Jinsi Takukuru ilivyowahoji wabunge Chadema

Muktasari:

Katika kipindi ambacho tovuti ya Mwananchi haikuwa hewani baada ya kufungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa muda wa miezi sita, moja ya matukio yaliyotikisa ni Takukuru kuwahoji wabunge wote wa chama cha Chadema.

Mwanza. Katika kipindi ambacho tovuti ya Mwananchi haikuwa hewani baada ya kufungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa muda wa miezi sita, moja ya matukio yaliyotikisa ni Takukuru kuwahoji wabunge wote wa chama cha Chadema.

Walihojiwa kutokana na malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za michango ya wabunge zilizotolewa na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao kwa sasa wamehamia vyama vingine vya siasa.

Uchunguzi huo ulioanza mwishoni mwa Mei, 2020 kwa kuanza kuwahoji wabunge wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania akiwemo David Silinde (aliyekuwa mbunge wa Momba), Peter Lijualikali (Kilombero), Joyce Sokombi na Suzan Masele ambao walikuwa wabunge wa Viti Maalum.

Juni 10, 2020  Takukuru kupitia kwa ofisa uhusiano wake, Doreen Kapwani ilitangazia umma na kuthibitisha kuwepo kwa uchunguzi huo.

Katika taarifa yake, Kapwani alisema wabunge 69 wa Chadema wangehojiwa kupata ukweli wa jambo hilo. Katika mahojiano hayo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ndio alikuwa wa mwisho kuhojiwa na taasisi hiyo.

Wengine waliokuwemo kwenye orodha ya kuhojiwa na Takukuru ni wajumbe wa Bodi ya Udhamini na viongozi wa Chadema, waliowahi kuwa wabunge wa chama hicho na maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa mujibu wa katiba na makubaliano maalum yanayosainiwa na wabunge wa Chadema, Wabunge wa Viti Maalum huchangia zaidi ya Sh1.5 milioni kila mwezi kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa chama, huku wale wa majimbo wakichangia Sh520, 000 kwa mwezi.

Wakati waliokuwa wabunge wa Chadema, Cecilia Paresso (Viti Maalum) na Suzan Kiwanga (Mlimba) walikaririwa wakibeza malalamiko hayo kwa hoja kuwa michango hiyo ni ya kikatiba, taarifa ya Takukuru kwa umma ilibainisha kuwa malalamiko hayo yakithibitika, wahusika wanaweza kukutwa na makosa mawili.

Akifafanua kwanini,  Takukuru inachunguza suala hilo linalodaiwa kuwa la kikatiba kwa Chadema, Kapwani alisema; “Tunafanya hivi kwa kuwa yanawezekana katika tuhuma hii kukapatikana makosa ya ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama na matumizi mabaya ya mamlaka,”

Hata hivyo hadi jana asubuhi Oktoba 15, 2020  hakukuwa na taarifa rasmi kwa umma imetolewa na Takukuru kuhusu kilichobainika na hatua inayofuata.

Akiongozana na mawakili wake wawili, Fredrick Kiwelo na John Mallya, Mbowe alihojiwa na maofisa wa Takukuru jijini Dar es Salaam Agosti 11, 2020.

Kabla ya Takukuru kuhitimisha mahojiano na wabunge, taasisi hiyo iliingia kwenye malumbano na uongozi wa Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu, John Mnyika baada chama hicho kikuu cha upinzani nchini kugoma kutoa nyaraka za ziada zilizoombwa na Takukuru.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mnyika alitangaza msimamo wa Chadema kutokabidhi nyaraka za ziada Takukuru kwa sababu hayana uhusiano na kilichokuwa kikichunguzwa tangu awali.

Katika mkutano wake na wana habari, Mnyika alisema chama chake kiko tayari kushirikiana na Takukuru katika uchunguzi wowote na kutoa nyaraka pale taasisi hiyo itakapoweka wazi jambo linalochunguzwa na sababu za uchunguzi huo kama ilivyofanya katika suala la michango ya wabunge.

Hata hivyo, msimamo huo wa Chadema ulipingwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo akisema unaweza kuwaingiza matatani wenye dhamana ya kutoa nyaraka hizo kwa kosa la kukwamisha taasisi hiyo kutimiza wajibu.

Kukiwa kumesalia siku chache Watanzania wamchague Rais, wabunge na madiwani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, hamu na shauku ya kujua matokeo ya uchunguzi wa Takukuru kuhusu tuhuma hizi inaongezeka.

“Kama walivyoutangazia umma kuwepo kwa uchunguzi; vivyo hivyo wanao wajibu wa kuujulisha umma nini kilichobainika kwa sababu fedha zinazochunguzwa matumizi yake zimetokana na kodi za wananchi,” anasema Edwin Soko, mchambuzi wa masuala ya kisiasa.

Akifafanua, Soko anasema; “Kama tuhuma zimethibitika umma ujue na hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria. Kama hakuna ushahidi wa tuhuma za ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama wala matumizi mabaya ya mamlaka, basi pia umma ujue,”