Kampuni ya Green Miles yaondolewa kwenye kitalu

Muktasari:

Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Longido imeiondoa kampuni ya Green Miles katika kitalu cha uwindaji cha Lake Natron (East) na kuifunga kambi ya kampuni hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Arusha. Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Longido imeiondoa kampuni ya Green Miles katika kitalu cha uwindaji cha Lake Natron (East) na kuifunga kambi ya kampuni hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kuondolewa kwa kampuni hiyo huenda kukawa mwisho wa mgogoro wa muda mrefu baina yake, vijiji 23  na Serikali.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumanne Januari 21, 2020 na katibu tawala wa Wilaya ya Longido, Toba Nguvila  aliyekuwa ameongozana na wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia utekelezaji  wa maagizo ya Serikali kuitaka kampuni hiyo kuondoka katika kitalu hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisa wa kikosi cha kupambana na ujangili (KDU) Mkoa wa Arusha, Emmanuel Pius alisema wameendesha operesheni ua kumuondoa kwa nguvu mwekezaji huyo baada ya kukaidi maagizo ya Serikali.

"Alitakiwa Januari 20 awe ameondoka lakini amekaidi hivyo kamishna wa Tawa (Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini) ameagiza tuje kumuondoa kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama Mkoa. Kitalu kitakuwa chini ya usimamizi wa Tawa,” alisema Pius.

Agosti 7, 2019 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla  alitangaza uamuzi wa Serikali kuiondoa kampuni hiyo kutokana na kukiuka taratibu za uwindaji.

Hata hivyo, kampuni hiyo iliomba kuongeza muda hadi Desemba 16, 2019  ili kukabidhi kitalu hicho kwa maelezo kuwa wakati uamuzi unatangazwa walikuwa na watalii wakiwinda.

Jumamosi Januari 18, 2020 mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe alisema  hivi karibuni katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda alitoa taarifa nyingine akiitaka kampuni hiyo kuondoka Januari 20, mwaka huu.

Kwa muda mrefu kampuni hiyo imekuwa na mgogoro na vijiji 23 vinavyozunguka kitalu hicho vinavyodai zaidi ya Sh350 milioni.

Pia, inadaiwa kukiuka taratibu za umiliki wa kitalu ikiwepo kushindwa kudhibiti ujangili baada ya twiga 16 kuuawa katika kitalu hicho, madai ambayo Awadh amekuwa akiyakanusha.