Kangi Lugola atinga Takukuru kuhojiwa na ilani ya CCM mkononi -VIDEO

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi, Kangi Lugola akiwasili katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) zilizopo Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa, leo asubuhi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

 Takukuru imemtanguliza Lugola kuhojiwa na imeelezwa atafuatiwa na Andengenye, Kingu na Masauni.

Dodoma. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) makao makuu jijini Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa.

Lugola amefika katika ofisi hizo leo Ijumaa Januari 30, 2020 saa 1.24 asubuhi akiwa katika gari ndogo aina ya Klugger rangi nyeusi na hakuingia nayo ndani ya geti.

Akiwa amevalialia kaunda suti nyeusi huku mkono wa kulia akiwa ameshikaiIlani ya CCM na mkoba mweusi, alionekana mwenye kujiamini zaidi na akielekea moja kwa moja  eneo la mapokezi ndani ya jengo hilo lililoko mtaa wa Jamhuri.

Moja ya maofisa wa Takukuru alimuongoza kuingia ndani ya jengo ambako alikwenda kukaa eneo la mapokezi mahali walipokuwa wamekaa waandishi na wakatakiwa kumpisha.

"Hata ninyi mpo huku, oh hata wewe nawe upo, haya hamjambo, habari zenu," alisalimia Lugola akipunga mkono uliobeba ilani ya CCM.

Mmoja wa maofisa wa Takukuru amesema baada ya Lugola kuhojiwa, saa 3.30 atahojiwa aliyekuwa Kamishina wa Zimamoto, Thobias Andengenye, saa 8.00 atahojiwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Jakob Kingu ambaye sasa ni balozi na saa 12 jioni atahojiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

Kuhojiwa kwa watumishi hao ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuhusu mkataba tata walioingia katika manunuzi ya vifaa vya zimamoto.