Kesi ya Halima Mdee yakwama kuendelea

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mde

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na ushahidi Katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kutokana na wakili wa upande wa utetezi kuwa kwenye kikao cha Chama cha Mawakili Tanganyika(TLS) Mkoani Arusha.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea na ushahidi Katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kutokana na wakili wa upande wa utetezi kuwa kwenye kikao cha Chama cha Mwakili Tanganyika(TLS) Mkoani Arusha.

Wakili wa Serikali, Estazia Wilson amedai hayo leo Jumatano Septemba 4, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi yupo mahakamani hapo lakini amepewa taarifa kuwa wakili wa utetezi ameenda mkoani Arusha kwenye kikao cha TLS.

"Kwa kuwa wakili anayemtetea Mdee ameenda kwenye kikao mkoani Arusha, naiomba mahakama hii ihairishe shauri hili ipange tarehe nyingine ya kuendelea na ushahidi," amedai Wilson.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 3, 2019 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.