Kete 321 zakamatwa Manyara, wawili mbaroni

Muktasari:

Jeshi la polisi mkoani Manyara linawashikilia watu wawili wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya kwenye eneo la mgodi wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mirerani. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara nchini Tanzania linawashikilia watu wawili wakidaiwa kukutwa na kete 321 za dawa ya kulevya kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite yaliyopo Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani humo.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Agostino Senga akizungumza na Mwananchi leo Septemba 13,2019 amesema dawa hizo za kulevya zinahisiwa ni aina ya Heroine.

Amesema watu hao wamekamatwa Septemba 11,2019 saa 10 jioni kwenye kitalu B (Opec) ndani ya ukuta unaozunguka mgodi wa madini hayo ya Tanzanite.

Amefafanua watu ambao majina yao yamehifadhiwa wamekamatwa kwenye jengo ambalo ujenzi wake bado haujakamilika na dawa hizo walizifunga kwenye vipakiti vidogo wakisubiri wateja wao.

"Baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanafanya biashara hiyo askari wetu walifika mara moja kwenye eneo la tukio na kuwakamata watu hao wakiwa na dawa hizo," amesema Kamanda Senga.

Kamanda Senga  amewataka watu wote wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta huo kuhakikisha wanajihusisha na kazi halali kwani wapo timamu kuhakikisha wanakomesha uhalifu katika eneo hilo.