Kigwangalla anogesha ziara ya wasanii

Muktasari:

Ziara ya wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya 'Bongo fleva' imeingia siku ya pili leo, ambapo wameendelea kutembelea vivutio vya utalii mjini hapa.


Tanga. Ziara ya wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya 'Bongo fleva' imeingia siku ya pili leo, ambapo wameendelea kutembelea vivutio vya utalii mjini hapa.

Ziara hiyo iliyoanzia wilayani Bagamoyo jana, leo wasanii hao wametembelea magofu ya Tongoni yaliyopo nje kidogo ya mji wa Tanga na mapango ya Amboni.

Katika ziara hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangalla ameungana nao kutembelea mapango ya Amboni ambako wamepatiwa maelezo yabayohusiana na maeneo hayo yanayobeba historia ya kale na ile ya asili.

Mhifadhi wa magofu ya Amboni, Ally Mbarouk amewaeleza wasanii hao katika ziara hiyo iliyo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuwa eneo hilo lina historia yenye miaka zaidi ya 500.

"Magofu haya yanayohusisha makaburi na msikiti ni majengo yaliyokuwapo miaka zaidi ya 500, na kwa hiyo yana historia ya kiutamaduni na maisha ya tamaduni za Kiarabu na Kiswahili," amesema.

Msanii wa filamu, Jacob Steven 'JB', ameutaka uongozi wa TFS kuyakarabati magofu hayo ili yasitoweke.

Naye Chegge Chigunda amesema historia muhimu za nchi zinapaswa kuhifadhiwa vizuri ili vizazi vijavyo viiikute ikiwa imara, huku Amin Mwinyimkuu akihimiza utalii endelevu wa Watanzania kuenzi ipasavyo kaulimbiu ya utalii wa ndani.

Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo amewataka wasanii hao kuendelea kuhimiza wananchi kutumia maeneo hayo kwa ajili ya kujifunza kutokana jamii zilizoishi miaka mingi hapa nchini.

Ziara hiyo inayolenga kuwawezesha wasanii kuwa mabalozi wa utalii wa ndani itamalizika kesho kwa kutembelea Hifadhi Asili ya Amani ambapo Dk Kigwangalla anatarajiwa kuzungumza na wasanii hao.