Kilichojiri kesi ya kumteka Mo Dewji mahakamani

Muktasari:

Upelelezi wa kesi ya kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Gullam Dewji, maarufu kama MO, inayomkabili Mousa Twaleb(46) na wenzake, bado haujakamilika.

 

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania,  Mohamed Dewji, maarufu MO, inayomkabili Mousa Twaleb (46) na wenzake, bado haujakamilika.

Twaleb ambaye ni dereva tax na mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam anakabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni  kutakatisha fedha kiasi cha Sh8 milioni,  kujihusisha na genge la uhalifu na kumteka nyara Mo Dewji.

Hata hivyo, tayari Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshatoa hati ya kuwakamata washtakiwa watano ili waunganishwe katika kesi hiyo.

Leo Jumanne, Septemba 3, 2019, Wakili wa Serikali, Daisy Makakala, ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika hivyo, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Makakala.

Pia, Makakala ameendelea kudai kuwa bado wanaendelea kuwatafuta washtakiwa watano ambao wataunganishwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 42/2019.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 16, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa  rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Twaleb, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  raia wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala na raia wanne wa Msumbiji ambao ni Henrique Simbue, Daniel Berdardo, Issac Tomu na Zacarious Junior.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg, nchini Afrika Kusini kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.

Pia  Oktoba 11, 2018 katika maeneo ya Hoteli ya Colloseum  iliyopo wilayani Kinondoni jiji hapa, Twaleb na wenzake ambao bado hawajafikishwa mahakamani, walimteka nyara Mohamed Dewji kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Julai 10, 2018 katika maeneo ya Mbezi Beach wilaya ya  Kinondoni, Twaleb na wenzake ambao bado hawajafikishwa mahakamani walitakatisha fedha kiasi cha Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.