Kiongozi wa upinzani Zimbabwe afananisha ukandamizwaji wa demokrasia Afrika na Corona

Muktasari:

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Movement Decratic Change (MDC) cha Zimbabwe, Tendai Biti ametumia hotuba yake kwenye mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, Tanzania kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwamo utawala bora.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Upinzani katika Bunge la Zimbabwe, Tendai Biti amesema wakati dunia iko katuika mshtuko wa ugonjwa hatari wa Corona, Bara la Afrika limekumbwa na ugonjwa wa ukandamizwaji wa demokrasia.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama cha ACT Wazalendo leo Jumamosi Machi 14, 2020 Biti anayetokea chama cha Movement Decratic Change (MDC), amevilaumu vyama vya ukombozi vya Afrika akisema vimepoteza malengo ya ukombozi na kubaki kukandamiza demokrasia.

“Nimesafiri kutoka Zimbabwe, nimepitia katika viwanja viwili vya ndege na kila nilipofika nimekuta wamevaa masiki (mdomoni), kutokana na ugonjwa wa Corona,” amesema Biti. 

“Lakini kuna ugonjwa wa kisiasa, wa kutovumilia, wa kidikteta uliojaa katika Afrika inaovuruga utu wetu,” amesema

Huku akitoa mfano wa nchi ya Zimbabwe, Biti amesema viongozi walioleta ukombozi wamebaki madarakani kwa muda mrefu wakikandamiza demokrasia.

“Nenda Zimbabwe ambako kwa miaka 38 tulitawaliwa kiimla na Robert Mugabe. Wakati Jeshi lilipomwondoa mwaka 2017 tulisherehekea, bika kujua kwamba tunaruka majivu ili tukanyage moto,” amesema.

“Miaka miwili baadaye Zimbabwe imejikuta kwenye janga lingine la udikteta usio na rangi wa mtu anayeitwa Emerson Nambudzo Mnangagwa.”

Huku akipongeza utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Biti amesema kumekuwa na tishio la utawala wa demokrasia nchini Tanzania.

“Tumeona watu wakikamatwa, waandishi wa habari wakikamatwa, tumeona makosa ya uchochezi yaliyokuwa yakitumiwa na wakoloni yakiwa makosa makubwa ya nchi hii. Baadhi ya wabunge wameshitakiwa na wametakiwa kulipa faini kubwa,” amsema. 

Ameendelea kusema, “Nina swali kwa wakombozi wote. Swali kwa ZANU PF, swali kwa Frelimo. MPLAS ya Angola, kwa ndugu zangu ANC, swali kwa CCM. Kwa nini baada ua kipindi cha uhuru, uzalendo umeshindikana?”