Kuchemsha chupa za watoto ni hatari, wasema wataalamu

Sunday September 15 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kama mifuko ya plastiki ilikuwa janga kwa mazingira, matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya plastiki ni janga jipya la afya, kwa mujibu wa wataalamu.

Kuanzia Juni mosi, matumizi ya mifuko ya plastiki yalipigwa marufuku kutokana na athari zake kwa mazingira pia baadhi ya mifugo, na adhabu kali zimewekwa kwa watakaokiuka agizo hilo.

Sasa vifaa vya plastiki, kama chupa za maji, chupa za maziwa za watoto, kontaina na vikombe vya plastiki, vinatakiwa kutumika kwa uangalifu kwa kuwa visipotumika kwa usahihi vinaweza kusababisha athari kama mvurugiko wa homoni na saratani.

Watafiti na wataalamu wa afya wameiambia Mwananchi kuwa zaidi ya asilimia 60 ya plastiki zinazozalishwa zina uhusiano wa moja kwa moja na chakula ikiwamo vyombo na chupa za vinywaji.

Kibaya na hatari zaidi ni imani kwamba kuchemsha chombo, hasa anavyotumia mtoto kwa chakula kama maziwa na uji, hukifanya kiwe safi zaidi.

Na hata wauzaji maziwa, asali, juisi na vinywaji vingine vinavyotengenezwa kienyeji, hutumia chupa za plastiki zilizokwishatumika.

Advertisement

Lakini wataalamu wanasema kufanya hivyo ni hatari na kunaweza kusababisha madhara makubwa kiafya.

Mkurugenzi wa mafunzo, tafiti, takwimu na uhamasishaji Osha, Joshua Matiko alisema wengi huchemsha vyombo vya watoto vya plastiki kwa nia ya kuua wadudu, lakini si sahihi kwa kuwa vina kemikali ambazo huyeyuka na baadhi ya watengenezaji huongeza kemikali nyingine.

Alisema matumizi ya vifaa vya plastiki kwa chakula kama vinywaji, maji, soda, chupa za maziwa za watoto na vyombo ni lazima yawe sahihi.

“Chombo chochote cha plastiki kikitumika vizuri hakina madhara. Chupa ya maji au kinywaji imetengenezwa ili kutumika mara moja. Wengi wanazitumia kuwekea tena juisi, mafuta ya kula, petroli au maziwa. Unapoitumia zaidi ya mara moja ina madhara,” alisema.

“Vivyo hivyo chombo cha plastiki hakipaswi kuwekwa kitu cha moto sana. Ukifanya hivyo huwa kinalainika na pale tayari hutoa kemikali ambazo ni hatari kiafya. Wengi wanaweka chakula cha moto au uji wa mtoto wanaupooza ukiwa humo, si sahihi.”

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto nyingi hasa kwenye kuzuia utengenezaji wa vitu vya plastiki kutokana na malighafi hizo kuwa rahisi kupatikana.

“Madhara mengine yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya plastiki ni kupata kisukari aina ya pili, unene kupindukia, saratani ya matiti na tezi dume, watoto kubalehe mapema, usonji na watoto kuchangamka kupita kiasi,” alisema Matiko.

Pia, alisema kuna ulazima wa kuangalia maelekezo ya vinywaji mfano maji ya chupa.

“Ila hatujali kuangalia ni aina gani ya plastiki iliyotunza maji. Aina ya plastiki huonyeshwa kwa kitu kinachojulikana kama resin identification code,” alisema.

“Katika kila plastiki unakuta alama ya pembetatu yenye namba kati ya 1 hadi 7 au maneno kama pete, HDPE, PVC katikati ya alama hiyo ya pembetatu.

“Alama hii ndiyo inakujulisha ni aina gani ya plastiki iliyotumika. Mara nyingi inakuwa chini kwenye kitako cha chupa au kifungashio.”

Matiko alisema inashauriwa kuepuka plastiki namba 3,7 na 6. wakati huohuo namba 1,2,4 na 5 ni salama japokuwa zinahitaji uangalifu.

Alisema kwa hapa nchini kaya nyingi zinatumia chupa za plastiki zaidi ya mara moja na huzihifadhi kwenye majokofu.

Naye mkurugenzi wa kinga kutoka Hospitali ya Saratani Ocean Road, Dk Crispin Kahesa alisema kuna uhusiano kati ya kemikali zinazotumika kutengenezea plastiki ziwe zile zinazotumika kwa chakula, na vifaa mbalimbali, na ugonjwa wa saratani.

Alisema kemikali hizo zinaweza kupitishwa kwa njia ya kula, harufu au mgusano.

“Katika tafiti zilizofanyika hakuna ushahidi wa moja kwa moja, lakini zinaonyesha kiasi cha kemikali hizo zinazoweza kuleta madhara kwa binadamu ni microgram 50,” alisema.

Dk Kahesa, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani alisema mara nyingi kemikali hizo zikiingia katika mwili wa binadamu huingilia mfumo wa ufanyaji kazi wa homoni.

“Husababisha ukosefu wa watoto, masuala ya uzazi, balehe, saratani ya maziwa na tezi dume, japokuwa wapo wanaopata matatizo kama hayo kutokana na sababu nyingine,” alisema.

Hata hivyo, alisema matumizi sahihi ya plastiki ndiyo yatakayomfanya mtumiaji kuwa salama.

Mkuu wa uhusiano Shirika la Viwango (TBS), Rhoida Andusamile alisema wana jukumu la kuthibitisha ubora wa bidhaa pamoja na vifungashio.

“Wazalishaji waliothibitisha ubora hutumia chupa ambazo hazijatumika, hivyo hakuna chupa za plastiki zilizotumika kwa bidhaa zilizothibitishwa ubora,” alisema.

Advertisement