Kupanda Mlima Kilimanjaro ni sawa na kwenda hospitali kuangalia afya

Muktasari:

Watanzania wamehimizwa kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kuwa kuna faida nyingi zaidi ya kutalii ikiwemo kutambua uimara wa afya zao.

Moshi. Watanzania wamehimizwa kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro, kwa kuwa kuna faida nyingi zaidi ya kutalii.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Septemba 26, 2019 na mwongoza watalii, Bruno Mkerenga alipokuwa akizungumzia umuhimu wa kupanda mlima huo katika mazoezi ya kuupandisha.

Mazeozi hayo yameshirikisha baadhi ya waandishi wa habari, wasanii wa muziki na filamu kwenye kampeni ya 'Kili Challenge Twenzetu Kutalii' iliyoandaliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamis Kigwangala kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya utalii akiwemo Miss Tanzania 2018, Elizabeth Makune.

Katika mazoezi hayo ambayo yalichukua takribani saa mbili kufikia geti la kuanza kupanda mlima huo, Mkerenga amesema kupanda mbali ya kuwa ni utalii, lakini mtu anajipima hali ya afya yake.

"Ukishapanda Mlima Kilimanjaro ni sawa na umekuja hospitalini kwani hapa ndio utagundua afya yako iko fiti au la,  kwani kuna hali mbalimbali za kimazingira mpaka unafika kileleni.” 

"Tusiwaache watu kutoka nje (ya Tanzania) waje wafaidi kupanda mlima huu, kwani una faida nyingi ukiachilia mbali kuwa ni sehemu ya utalii, pia inaimarisha afya zetu," amesema Mkerenga.

Wasanii wanaofanya mazoezi kwa ajili ya kupanda mlima huo ni pamoja na Dude, Maya, Husna Sajenti,  Richie Richie, Shetta, Amino, Ebitoke, AT kutoka visiwani Zanzibar, Kety, Maya na Mariam Ismail.