Kuwasilisha kero, malalamiko Dar sasa kwa ujumbe wa simu ya mkononi

Wednesday October 09 2019
pic makonda

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na watendaji wa mkoa huo kuhusu mfumo mpya wa kupokea malalamiko na kero za wananchi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa  wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wakazi wa mkoa huo                                                                                                                                                                                                                                                                       hawatalazimika kwenda ofisi za Serikali kutoa kero zao badala  yake watazitoa kwa simu zao za mkononi.

Amesema mfumo wa uratibu malalamiko ya wananchi na uwajibikaji wa watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, utasaidia kuokoa gharama za wananchi walizokuwa wakitumia kwenda kwenye ofisi mbalimbali kutoa kero zao, licha ya muda mwingine kutowakuta wahusika.

Ofisa wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Dar es Salaam, Upendo  Charles amesema namba za kutoa kero au malalamiko zimegawanywa kuanzia ngazi ya halmashauri, kata na mkoa.

"Ukitaka kutuma kero au malalamiko utachukua simu yako unakwenda sehemu ya kuandika ujumbe na kuandika neno DSM, namba ya ngazi husika (kata, halmashauri na Mkoa) kisha utapokea ujumbe mfupi wa namba utakayotumia kufuatilia kama maombi uliyoomba yameshughulikiwa au la," amesema

Makonda amezindua mfumo huo leo Jumatano Oktoba 9, 2019 mbele ya watendaji mbalimbali wa mkoa huo  akisema hatua hiyo ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi ya kuwarahisishia  huduma wananchi wa mkoa huo.

" Ilikuwa ndoto yangu baada ya kuona watu wengi wakikaa ofisini wakitafuta majibu kwa mambo  yanayoweza kutatuliwa kwenye ngazi ya mtaa au kata. Mfumo huu utawasaidia na hakutakuwa na gharama wakati wa kutuma kero au malalamiko yao," amesema Makonda.

Advertisement

Makonda amefafanua kuwa Dar es Salaam, imeunganisha na mtandao na taarifa za kero na malalamiko yatakayotumwa na wananchi zitakwenda moja kwenye idara husika na viongozi husika wataziona.

" Utapewa taarifa ya mwenendo wa jambo lako ulilowasilisha bila usumbufu wa kwenda katika ofisi husika. Usumbufu wa kuja ofisini utapungua badala yake utapata huduma ukiwa nyumbani kwako.”

"Kama jambo litahitaji ushahidi, utapigia simu kwenda ofisi husika kwa lengo la kutoa ushirikiano," amesema Makonda.

Amesema mfumo huo utasaidia kujua kiwango cha uwajibikaji kwa idara mbalimbali  na kila mwezi itakuwa ikitolewa taarifa ya hali ya tathmini kwenye idara hizo.

Advertisement