Laini za simu milioni 12 zasajiliwa hadi sasa Tanzania

Muktasari:

Serikali imesema usajili wa laini za simu unakwenda vizuri lakini wenye simu wameitwa kusajili kwani muda ukifika  mitambo itazimwa

Dodoma. Zikiwa zimebaki siku 54 ili kufunga usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole, hadi leo Watanzania milioni 12.783 tayari wamesajili laini zao.

Takwimu hizo zimetolea bungeni leo Alhamisi Novemba 7,2019 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atashasta Nditiye ambaye ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kusajili laini zao kwani muda ukifika, laini zao hazitakuwa hewani.

Nditiye alikuwa anajibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zainab Katimba ambaye aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuwasaidia Watanzania ikiwamo watu wa Kigoma ili kupata vitambulisho vya taifa kwa ajili ya kusaidia usajili wa laini zao.

"Hali inakwenda vizuri nchi nzima, tumefanikiwa kwa idadi kubwa lakini niwaombe Watanzania wote wenye laini wakasajili kwani muda ukifika tutazima mitambo na hawatakuwa na mawasiliano," amesema Nditiye

Naibu waziri amesema usajili unakwenda vizuri na kinachotakiwa katika usajili siyo kitambulisho cha taifa, bali namba za usajili wa vitambulisho vya taifa.

Kuhusu mawasiliano na ufungaji minara, Nditiye amesema wameendelea kufanya vizuri na juhudi za kufunga minara maeneo yasiyo na mawasiliano na akaomba wabunge kupeleka orodha ya maeneo ambayo wangehitaji kufunga minara.