Lipumba aahidi kumaliza tatizo la ajira Tanzania

Mgombea urais kupitia CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

Muktasari:

Mgombea urais kupitia CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema akichaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi  atahakikisha anamaliza changamoto ya ajira nchini Tanzania.

Nanyamba. Mgombea urais kupitia CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema akichaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi  atahakikisha anamaliza changamoto ya ajira nchini Tanzania.

Amesema miongoni mwa ajira atakazotoa ni kuziba nafasi za watumishi wa serikali walioondolewa kwa madai ya kuwa na vyeti feki pamoja na za watumishi waliostaafu na kufariki dunia.

Amedai nafasi hizo hazijajazwa  jambo ambalo linasababisha uhaba wa watumishi katika sekta ya afya na elimu.

Ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mji mdogo wa Mahuta Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

"Sasa hivi watu wanasema vyuma vimekaza na hii inatokana na sera ya serikali, wafanyakazi hawajaongezewa mishahara idadi ya wafanyakazi haiongezwi kwenye sekta muhimu kama afya na elimu," amesema Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi.

"Wapo watumishi  walioondolewa na serikali kwa madai ya kuwa na  vyeti feki lakini nafasi zao hazijajazwa na watu wengine, pia wapo  waliomaliza masomo yao ya udaktari hawajapata ajira pamoja na kwamba tuna upungufu wa wauguzi na madaktari. Wapo walimu nao hawajapata ajira pamoja na kwamba hatuna walimu wa kutosha.”

Ameongeza, “endapo mtanichagua kuwa rais wenu nitahakikisha ajira zinapatikana hasa kwa kuziba nafasi za watumishia waliofariki na wengine waliostaafu. Hizi  nafasi zipo lakini hazijazibwa na watu wengine.”