Lissu: Sirejei Tanzania kwa sasa, mazingira ya usalama wangu si mazuri

Muktasari:

  • Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema hawezi kurejea Tanzania kwa sasa kwa kuwa mazingira ya usalama wake si mazuri.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema hawezi kurejea Tanzania kwa sasa kwa kuwa mazingira ya usalama wake si mazuri.

Lissu ametoa kauli hiyo jana Jumatano Oktoba 9, 2019 katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA) baada ya kuulizwa swali na mtangazaji Mwamoyo Hamza kuhusu mpango wake wa kurejea nchini baada ya kumaliza matibabu.

Kauli hiyo ni tofauti na aliyotoa Septemba 7, 2019 kuwa atarejea Tanzania “mchana kweupe” akitokea Ubelgiji alikoenda kutibiwa, akisema suala hilo halitakuwa siri kama ambavyo anashauriwa na watu wengi. Alitoa kauli hiyo katika andiko lake lenye kichwa cha habari kisemacho “Miaka Miwili ya Mateso, Matumaini”.

“Nimeshakamilisha tiba kwa hiyo sababu ya kiafya ya kuendelea kukaa Ubelgiji haipo tena, iliyobaki sasa ni viongozi wenzangu (wa Chadema) waliopo Tanzania waniambie mazingira yapo sawasawa ya kiusalama ya mimi kurudi,” alisema.

“Kumbuka wale walionipiga risasi 16 mchana wa saa saba bado wanaitwa watu wasiojulikana.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa Ubelgiji kukamilisha matibabu na hadi sasa yuko nchi hiyo ya barani Ulaya.

Alipoulizwa na Hamza sababu za kubadili mpango wake wa kurejea Tanzania, Lissu alisema: “Nimebadili kauli kwa sababu za wazi nilizozisema. Mazingira ya kiusalama si mazuri. Kuna maneno yanajitokeza kwenye mitandao ya kijamii kwamba ngoja aje mara hii hatutakosea shabaha. Sasa katika mazingira haya watu wenye busara wakasema hebu tuangalie hali ya usalama.”

Alipoulizwa kama ataendelea kuishi ughaibuni kutokana na kuhofia usalama wake, alisema: “Hapana  siwezi nikakwama kurudi nyumbani.”

Kuhusu afya yake, mwanasheria huyo wa kujitegemea alisema tangu Juni 29, 2019 aliacha kutembea kwa msaada wa magongo.