Lissu akwamisha kesi yake ya uchochezi kuendelea

Monday June 24 2019

 

By Pamela Chilongola,Mwananchi [email protected] mwananchi

Dar es salaam. Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wenzake watatu imeahirishwa baada ya mbunge huyo kuendelea na matibabu nje ya nchi.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi..

Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde amedai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Juni 24,2019 amedai shauri lilikuja kwa ya kutajwa aliomba ipangwe tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema washtakiwa wote wataendelea na dhamana yao na  shauri hilo limeahirishwa hadi Julai 24, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Advertisement

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Advertisement