Liverpool yahamia uwanja wa kisasa wa mazoezi

Muktasari:

Mabingwa hao wa soka wa England wamehama uwanja wa Melwood ambao wameutumia kwa zaidi ya miaka 70 na sasa wanakwenda eneo walilolitengeneza kisasa kwa gharama za zaidi ya Sh130 trilioni.

Jurgen Klopp leo ameaga kwa hisia uwanja wa mazoezi wa kihistoria wa klabu ya Liverpool wa Melwood wakati vinara hao wa Ligi Kuu wakijiandaa kuhamia makao mapya.

Melwood imekuwa sehemu muhimu ya klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 70, huku vizazi tofauti vilivyopitia Anfield vikinoa makali yao kwenye viwanja vya mazoezi.

Lakini, ikiwa haiwezi kuendeleza zaidi eneo hilo, Liverpool itahamia katika eneo jipya la mazoezi, AXA Training Centre, lililojengwa Kirbym nje kidogo ya jiji la Liverpool kwa gharama ya dola 66 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh130 trilioni za Kitanzania), kuanzia wiki ijayo.

Eneo hilo jipya la mita 9,200 za mraba limetengenezwa kwa ustadi mkubwa, likiwa na viwanja vitatu vya mazoezi, ukumbi wa michezo ya ndani, gym mbili, bwawa la kuogelea, mfumo wa tiba ya maji na vifaa vya mazoezi kwa majeruhi wanaoanza kupona.

Melwood iliuzwa mwaka jana kwa kampuni ambayo itajenga nyumba za makazi eneo hilo.

Klopp na benchi lake la ufundi walienda kwa ajili ya kufunga milango ya eneo hilo, moja ya viwanja maarufu vya mazoezi duniani.

"Hisia tofauti, hisia tofauti hasa. Nafurahia kwenda Kirkby na nina huzuni kuondoka Melwood, kusema ukweli," Klopp aliandika katika tovuti ya Liverpool.

"Ni kitu cha ajabu; sikufikiria vizuri kuhusu kitu hiki, lakini nadhani msaidizi wangu binafsi ameshahamisha vitu vyangu vyote kutoka ofisini, kwa hiyo naelewa hatua kwa hatua kwamba sehemu hii tayari inaonekana tofauti.

"Nitapakumbuka sana, lakini hivi ndivyo hali inatakiwa iwe. Melwood ilikuwa nzuri hasa, ilikuwa ni sehemu muhimu -- sehemu muhimu katika maisha yangu, kw ahiyo nitapakumbuka. Lakini Kirkby itakuwa nzuri sana."