Lori laziba barabara Singida- Dodoma

Wednesday October 23 2019

Gari la mizigo lililoshindwa kupanda mlima

Gari la mizigo lililoshindwa kupanda mlima Salanda katikati ya Dodoma na Singida hali iliyosababisha kurudi nyuma kisha kuifunga barabara hiyo. Tangu saa 11.20 jioni hakuna gari linalopita kutoka uelekeo wa Dodoma au Singida. Picha na Mpigapicha wetu 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mamia ya abiria na watumiaji wa barabara ya Dodoma- Singida nchini Tanzania wamekwama eneo la Salanda baada ya lori la mizigo kuziba barabara hiyo.

Lori hilo lilishindwa kupanda mlima Salanda na kuanza kurudi nyuma na kusimama katikati ya barabara hali iliyosababisha magari kushindwa kupita.

Hali hiyo imesababisha abiria waliokuwa wakienda mikoa mbalimbali kwa kutumia barabara hiyo pamoja na  malori ya mizigo kukwama kuanzia saa 11 jioni leo Jumatano Oktoba 23, 2019.

Hadi saa 12:00 lori hilo lilikuwa halijaondolewa katika barabara hiyo.

Baadhi ya magari yanayotoka Singida kwenda Dodoma yalichepuka pembeni ya barabara hiyo na kupita katika shimo huku  yanayotokea Dodoma kwenda Singida yakilazimika kusubiri hadi lori hilo litakapotolewa.

Mmoja wa abiria anayetoka Kahama mkoani Shinyanga kwenda Morogoro, Mussa Msafiri ameiomba Serikali kuwasaidia ili kuliondoa gari hilo.

Advertisement

"Serikali hasa Jeshi la Polisi tunaliomba kama linasikia lije kuondoa lori hili bila hivyo hatutatoka hapa," amesema Msafiri

Advertisement