VIDEO: Lowassa, Pinda walivyozungumzia miaka 10 ya urais

Muktasari:

Wakati Edward Lowassa akitamani Rais John Magufuli kuongoza kwa miaka 10 akiamini nchi itapiga hatua kubwa katika maendeleo, Mizengo Pinda ameonyesha matamanio  yake ya kumuongezea miaka mitano zaidi lakini akikiri kuwa suala hilo ni gumu kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Dar es Salaam. Kwa nyakati tofauti mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Mizengo Pinda wamezungumzia miaka 10 ya urais.

Wakati Lowassa akitamani Rais John Magufuli kuongoza kwa miaka 10 akiamini nchi itapiga hatua kubwa katika maendeleo, Pinda ameonyesha matamanio  yake ya kumuongezea miaka mitano zaidi lakini akikiri kuwa suala hilo ni gumu kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Lowassa aliyekuwa waziri mkuu mwaka 2005 hadi 2008 alitoa kauli hiyo Jumatatu Desemba 9, 2019 alipopewa nafasi na Rais Magufuli kutoa salamu katika maadhimisho na miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015 na hadi leo Ijumaa amefikisha miaka minne na siku 38 katika uongozi.

"Kama Rais Magufuli akipewa nchi hii kwa miaka 10 itakuwa ya ajabu na mabadiliko makubwa mno," amesema Lowassa aliyehama CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chadema ambako alipitishwa kugombea urais mwaka 2015 na kushika nafasi ya pili nyuma ya Rais Magufuli.

Jana katika mkutano wa majadiliano ya Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika mjini Mwanza, Pinda alitumia maneno yake kwa uangalifu wakati akizungumzia mafanikio ya Rais Magufuli, akionyesha matamanio yake ya kumuongezea miaka mitano zaidi.

Pamoja na kwamba ndio kwanza Rais Magufuli anaelekea mwisho wa kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano, mjadala kuhusu kumuongezea muda, umekuwa ukiibuka kila mara. Jana, suala hilo lilijitokeza ndani ya mkutano wa majadiliano wa Halmashauri Kuu ya CCM.

“Mimi napata matumaini makubwa sana kwamba miaka hii kumi uliyopewa itatupeleka pazuri sana,” alisema Pinda akimuangalia Rais Magufuli aliyekuwa amekaa mbele.

“Ni kwa kuwa tu katiba zenyewe kidogo ziko tight lakini kama si kwa sababu hiyo, wallah ningesema mzee piga mingine tena, ongeza kama mitano tu.

 “Sasa najua hata mkijaribu kumlazimisha atawakatalia tu, lakini nataka niseme kwa namna ninavyoguswa na kazi kubwa unayoifanya; ni matumaini yetu kwamba katika kipindi hiki hata kama utatugomea kabisa kuongeza kidogo lakini utahakikisha basi umetupa kiongozi mwingine mzuri.”