Lowassa azungumzia migogoro wafugaji na wakulima, aipongeza Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania pamoja na taasisi za dini kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania pamoja na taasisi za dini kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 22, 2019 katika ibada ya shukrani ya Askofu Jacob Mameo Ole Paulo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) jimbo la Morogoro ya kutimiza miaka 25 ya ndoa na 25 ya uchungaji.

Ibada hiyo imefanyika usharika wa Bungo, Morogoro mjini na kuongozwa na mkuu wa kanisa hilo, Dk Fredrick Shoo

Lowassa ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2015 aligombea Urais kwa tiketi ya Chadema na kushika nafasi ya pili nyuma ya Rais John Magufuli  amesema vurugu kati ya wafugaji na wakulima mkoani humo hivi sasa hazipo.

"Zamani ilikuwa ukifuatilia vyombo vya habari unasikia migogoro ya wafugaji na wakulima hapa Morogoro. Kwa sasa hali ni shwari, ninawaomba viongozi na waumini wote tuendelee kuuombea Mkoa huu uzidi kuwa na amani na mshikamano,” amesema Lowassa.

Dk  Shoo amesema Askofu Mameo amekuwa mstari wa mbele katika usuluhishi wa migogoro ya wakulima na wafugaji  mkoani Morogoro.