Lukuvi amsimamisha kazi ofisa ardhi aliyetajwa na Rais Magufuli

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amemsimamisha kazi ofisa ardhi wa Wilaya ya Kigamboni ambaye siku tano zilizopita Rais John Magufuli alitaka achukuliwe hatua kwa kuwa haonekani kazini.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania, William Lukuvi amemsimamisha kazi ofisa ardhi wa Wilaya ya Kigamboni ambaye siku tano zilizopita Rais John Magufuli alitaka achukuliwe hatua kwa kuwa haonekani kazini.

Lukuvi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 17, 2020 wakati akikabidhi ekari 715 za ardhi kwa manispaa ya Kigamboni kama alivyoagizwa na Rais Magufuli wakati akizindua ofisi za mkurugenzi, mkuu wa wilaya ya Kigamboni pamoja na hospitali ya wilaya hiyo.

Siku hiyo Magufuli alisema, “nina tatizo na ofisa ardhi wa Kigamboni ni mtoro na hajafanya kazi karibu miezi mitatu, aliandikiwa barua na Wizara ya Ardhi ili ashughulikiwe ila bado wizara wanaleta mshahara wake. Najua wizara watafikishiwa ujumbe, kama ni mtoro atoroke kabisa, sifahamu mkurugenzi mmechukua hatua gani kwa ofisa ardhi huyo ambaye hafanyi kazi.”

Katika maelezo yake ya leo, Lukuvi amesema mtumishi huyo amesimamishwa kazi.

"Bahati nzuri  tulishapata barua kutoka kwa mkurugenzi wa Kigamboni na tumeshamsimamisha kazi wakati hatua za kinidhamu zikiendelea .Kama kutakuwa na uhitaji tutaleta mtu mwingine," amesema Lukuvi.