MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba aandika barua UN, aeleza anavyoteswa-9

Muktasari:

Pamoja na kwamba majeshi ya Umoja wa Mataifa yalikuwa Congo kulinda usalama, hayakuingilia kati kwa muda wote ambao Patrice Lumumba alikuwa akiteswa. Huenda hii ni kwa sababu Ubelgiji na Marekani hazikumtaka Lumumba. Akiwa mahabusu alifanikiwa kuandika barua mbili kwa msaada wa wanajeshi waliokuwa wakimtii. Endelea…

Jumamosi ya Desemba 3, Patrice Lumumba alihamishwa na wanajeshi na kupelekwa kambi ya Hardy iliyoko Thysville. Kwa mujibu wa waandishi wa habari waliokuwapo wakati wa kuhamishwa huko, Lumumba alionekana kuwa na maumivu makali kiasi kwamba alipata shida kupanda lori, na uso wake ulikuwa na alama za vipigo.

Kambi hiyo ilikuwa chini ya Kanali Louis Bobozo. Bobozo, ambaye ni mpwa wa Mobutu, baadaye akawa mkuu wa majeshi ya Congo kuanzia 1965 hadi 1972. Alikuwa ni sajenti tu wakati Congo ikipatia uhuru lakini alipandishwa vyeo haraka.

Katika kambi hiyo kulikuwa na mahabusu wengine wa kisiasa, mmoja wao ni Georges Grenfell ambaye alikuwa waziri katika serikali ya Lumumba.

Aliyekuwa mwakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Congo, Balozi Rajeshwar Dayal, aliandika kuhusu hali ya Lumumba. “Inasemekana ana maumivu makali yanayotokana na majeraha aliyopata alipowasili. Kichwa kimenyolewa nywele na bado mikono yake imefungwa kwa nyuma. Amefungiwa kwenye mahabusu ambayo haina hadhi ya utu na ni hatari sana kwa afya,” aliandika.

Telegramu ambayo Dayal alimtumia katibu mkuu wa UN, Dag Hammarskjold Desemba 5, iliripoti mazungumzo yaliyofanyika.

“Wanajeshi wa Morocco walioko UN Congo kambi ya Thysville wameripoti kuwapo majadiliano makali kati ya ANC (Jeshi la Congo) kuhusu wanavyomtendea Lumumba. Mabishano hayajatulia,” alisema.

Desemba 22, Dayal alituma ujumbe mwingine kwenda UN ukisema: “Uhalifu unaoendelezwa kwa Lumumba umeanza kuwakera (Kasavubu na Mobutu) kwa sababu umeanza kuwagawa wanajeshi.”

Januari 4, 1961, zikiwa ni siku 13 kabla ya kifo chake, Lumumba alifanikiwa kupenyeza barua mbili kutoka rumande. Ya kwanza ilikuwa ni ujumbe kwa viongozi wa UN, ambayo alieleza hali halisi ya mahabusu ya Camp Hardy.

“Niko hapa na wengine saba waliokuwa wabunge, miongoni mwao ni rais wa seneti, M. Okito (akimaanisha Joseph Okito) mfanyakazi wa serikali na dereva. Jumla yetu tuko 10. Tumewekwa hapa tangu Desemba 2, 1960. Chakula tunacholetewa mara mbili kwa siku ni kibaya sana,” aliandika Lumumba.

“Kwa siku nne sijala zaidi ya ndizi. Nimemweleza daktari wa Msalaba Mwekundu aliyeletwa kuniona; kanali wa Thysville alikuwapo. Nimetaka niletewe matunda ... Ingawa daktari aliruhusu, wanajeshi wa hapa wamekataa wakisema wana amri kutoka juu, kwa Kanali Mobutu.

“Madaktari wameelekeza tutembee [mazoezi] kila jioni nje ya mahabusu, lakini kanali na mkuu wa wilaya wamekataa. Nguo nilizovaa kwa siku 35 hazijaoshwa. Nimezuiwa kuvaa viatu. Kwa ufupi tunaishi katika hali isiyovumilika. Zaidi, sijapata taarifa zozote za mke wangu na familia yangu na sijui waliko. Nilipaswa nitembelewe naye, kama ilivyo katika sheria za Congo.”

Katika barua ya pili aliyomtumia mpwa wake aliyeitwa Albert Onawelo, Lumumba alitoa maelezo ya ziada kuhusu hali yake, pia akaelezea msaada fulani alioupata kutoka kwa baadhi ya wanajeshi.

“Niko hapa na wasaidizi saba, mmoja wao ni Joseph Okito. Tumefungiwa mahabusu gizani mfululizo tangu Desemba 2, 1960. Chakula tunachopewa (chikwangue na wali) unakera na ni kichafu na naweza kukaa siku tatu hadi nne bila kula. Kwa kweli hali ni mbaya kuliko hata wakati wa ukoloni. Kama akitokea askari akatupa ndizi za ziada, anakamatwa na kuadhibiwa. Pamoja na tabu zote kuna baadhi ya wanajeshi wanakuja kwa siri kunisaidia,” aliandika.

Mwisho wa barua hiyo, Lumumba alionyesha pia kuhusu mke wake wa tatu, Pauline Kie “anaendelea vizuri na hufika kila mara na kuwaachia ujumbe (wa Lumumba) wanajeshi walio upande wetu”.

Mwanzoni mwa Januari 1961, katibu mkuu wa UN, Dag Hammarskjold alizuru Congo na kujikuta akipokewa kwa maandamano ya wafuasi wa Lumumba.

Wakati mwanaharakati Cleophas Kamitatu alipojaribu kumpa Hammarskjold barua kutoka kwa Lumumba iliyoelezea hali katika mahabusu walimoshikiliwa, alionyesha kukasirika na kumwelekeza ampatie msaidizi wake.

Kamitatu, kwa kukasirishwa na majibu aliyopewa na Hammarskjold, naye aliandika barua yake yenye maneno yanayofanana na yale ya Lumumba.

“M. Lumumba amekuwa akiteswa kikatili kwa siku 35. Kwa siku zote hizo ameruhusiwa kuoga mara tatu tu. Anapewa chakula kinachostahili kupewa mbwa... Nguo alizovaa zimekaa mwilini kwa siku 35. Anaishi shimoni. Hakuwahi kufikishwa mahakamani, na hata mkewe amezuiwa kumwona,” aliandika.

Ingawa barua hizo ziliwafikia maofisa wa UN nchini Congo, hawakuchukua hatua yoyote kurekebisha hali ya mambo.

Hali ya wasiwasi ilikuwa ikizidi kutanda katika kambi aliyowekwa Lumumba na wenzake. Msaidizi wa Kanali Bobozo, Luteni Jacques Schoonbroot, alikuwa anasisitiza kuwa ghasia zinazozuka zinasababishwa na itikadi za kisiasa na kwamba kulikuwa na kikundi cha wanajeshi wa Congo katika kambi hiyo kilichomtii Lumumba.

Jumanne, Desemba 27 Kanali Bobozo aliarifiwa na msiri wake kuwa huenda Lumumba angetoroka au kutoroshwa. Aliamua mwenyewe kwenda kumfungia Lumumba na kuondoka na funguo.

Siku hiyo usiku alikwenda tena mwenyewe mahabusu alimofungiwa Lumumba kuwazuia makumi ya wanajeshi waliokuwa wamepanga kumtoa.

Kwa mujibu wa Luteni Schoonbroot kama alivyokaririwa na kitabu cha “Assassination of Lumumba”, Kanali Bobozo aliwaambia wanajeshi hao akisema “nyiye hamna la kufanya. Kama mnataka kumuachia mfungwa yeyote, labda muanze kwanza kuniua mimi.” Baada ya kauli hiyo, wanajeshi hao walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine.

Siku iliyofuata walikamatwa baadhi ya wanajeshi kutokana na jaribio lao la kumtoa Lumumba mahabusu. Baadaye ukazuka uvumi kwamba Lumumba alikuwa anatendwa vizuri mahabusu na alikula sikukuu ya Krismasi na maofisa wa kambi hiyo.

Luis Lopez Alvarez, raia wa Hispania aliyekuwa rafiki wa karibu na Lumumba, alikaririwa na Stephen Weissman katika kitabu cha “American Foreign Policy in the Congo 1960-1964”, akisema Lumumba alimlaumu sana balozi wa Marekani Congo kwa kuonekana kukaa upande wa watesi wake.

Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Ubelgiji ilikuwa na hofu sana na Lumumba kiasi kwamba ilituma ujumbe wa telegramu kwenda Kinshasa ikiwasisitiza “watilie maanani hatari ambayo ingesababishwa na Lumumba ikiwa ataachiwa huru”. Siku iliyofuata ukatumwa ujumbe kwa njia ya telegramu kutoka Congo kwenda Ubelgiji ukisema serikali ya Mobutu isingeruhusu Lumumba kuachiwa huru.

Muda mfupi baadaye, maofisa wa Congo mjini Kinshasa walianza kutafuta namna ya kumpoteza kabisa Lumumba.

Jumapili ya Januari 8, 1961, wanasiasa wawili wa Congo; Albert Delvaux na Cyrille Adoula walikwenda Katanga kuzungumza na rais wa eneo hilo, Moise Tshombe, kuhusu kumhamishia Lumumba huko.

Siku iliyofuata, wanasiasa wa Congo walishauriana na Rais Joseph Kasavubu na mkuu wa majeshi, kumhamisha Lumumba. Kamishna wa Ulinzi wa Congo, Fredinand Kazadi alisema kuhamishwa kwa Lumumba ni kwa muhimu sana ili kuepusha machafuko yaliyokuwa yananukia Thysville.

Siku iliyofuata, kamishna wa mambo ya ndani, Damien Kandolo, aliondoka kwenda Boma kwa ajili ya maandalizi hayo. Ubelgiji ilikuwa ikifuatilia kwa karibu hatua zote hizi.

Kulingana na simulizi za G. Heinz na H. Donnay katika kitabu cha “Lumumba: The Last Fifty Days”, aliyekuwa kiungo kati ya watesi wa Lumumba na serikali ya Ubelgiji ni Andre Lahaye, Mbelgiji aliyekuwa mshauri mkubwa wa mkuu wa Idara ya Usalama ya Congo, Victor Nendaka.

Aliyesaini barua ya kumtaka Nendaka amtoe Lumumba Thysville na kumpeleka Katanga ni Rais Kasavubu. Mpango wa usafiri wa ndege uliandaliwa na Kandolo Damien.

Kuanzia hapo Lahaye alifanya kazi kubwa akituma taarifa za mara kwa mara na hatua kwa hatua kwenda Brussels kwa lengo la kuelezea namna Lumumba alivyokuwa anashughulikiwa.

Itaendelea kesho...