MAKALA YA MALOTO: Ukiulizwa Nyerere ni nani, jibu ni lilelie “Baba wa Taifa”

Wednesday October 9 2019

 

By Luqman Maloto

Umewahi kujiuliza nafasi ya Tanzania ingekuwa wapi katika historia ya ukombozi wa bara la Afrika bila Mwalimu Julius Nyerere?

Je, akina Nelson Mandela, Thabo Mbeki, Jacob Zuma na wengine wangemiliki hati za kusafiria za Tanzania kwa nyakati tofauti ili kupata urahisi wa kusafiri nchi mbalimbali kusaka kuungwa mkono harakati zao kupata ukombozi dhidi ya utawala wa kibaguzi Afrika Kusini?

Mwaka 1962, kama Tanzania isingekuwa na Mwalimu Nyerere, kiongozi wa upinzani, Kenya, Raila Odinga, angepata wapi nafasi ya kwenda Ujerumani masomoni? Baada ya kunyimwa fursa ya kusafiri na Waingereza, Raila alikimbilia Tanganyika, Nyerere alimuwezesha. Mwalimu alikuwa kimbilio la kila Mwafrika aliyeonewa na wakoloni.

Wapigania uhuru wa Msumbiji, wangesafiri vipi duniani kwa kutumia hati za kusafiria za Tanzania, kama nchi isingekuwa na Mwalimu? Suala si kutoa hati, bali uthubutu wa kufanya hivyo. Mwaimu aliwathibitishia wakoloni kuwa hakuwa mwoga. Alipenda uhuru wa Waafrika kuliko hofu ya vitisho vyao. Aliwasaidia Waafrika bila woga.

Angola mpaka Namibia, aliipigania Zimbabwe, alitumia kila rasilimali kuhakikisha Afrika, hakuna nchi inabaki chini ya ukoloni. Aliasisi Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), alikuwa sababu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi za Kusini ya Afrika (SADC).

Huwezi kuitaja historia ya ukombozi wa Afrika bila Tanzania. Ni kwa sababu Tanzania ilikuwa na Mwalimu Nyerere.

Advertisement

Kamati ya Ukombozi wa Afrika, makao yake makuu kuwepo Dar es Salaam, Tanzania, haikuja kama ajali. Bali dhamira ya muda mrefu. Tangu Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Nyerere alichagua kutumia uhuru wa nchi kuipigania Afrika.

Maneno machache ya wakati wa uhuru, aliposema: “Sisi watu wa Tanganyika. Tungependa kuwasha mwenge kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Ung’are kupita mipaka yetu. Uwape matumaini waliokata tamaa. Ulete upendo palipokuwa na chuki. Utu ambako kulikuwa na kutwezwa. Hatuwezi, tofauti na nchi nyingine kutuma roketi mwezini, lakini tunaweza kutuma roketi za upendo na matumaini kwa ndugu zetu popote walipo.”

Lilikuwa tamko la nyakati ambazo, Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy, aliingia madarakani na tamko la kwenda mwezini. Wao walikuwa na uchumi mkubwa. Tanganyika haikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, ila ambacho kilikuwa ndani ya uwezo ni kuwapa upendo Waafrika Kusini weusi waliokuwa wakichukiwa na makaburu kisha kuwapa matumaini na heshima.

Ikawa sababu ya Tanganyika kugomea mwaliko wa kujiunga Umoja wa Madola kwa sababu ndani ya jumuiya hiyo ilikuwapo Afrika Kusini yenye kubagua watu weusi. Mwalimu Nyerere alisema: “Tunaamini kuwa uanachama wa Afrika Kusini chini ya mazingira ya sasa ni mzaha kwa muundo wa jumuiya unaotaka kusiwepo ubaguzi wa rangi. Hatuwezi kujiunga na umoja wa kirafiki ambao unahusisha dola ambayo kwa makusudi inatekeleza ubaguzi wa rangi bila huruma.”

Nani alitegemea nchi changa kama Tanganyika ingeweza kugomea uanachama wa Jumuiya ya Madola, kisha kupaza sauti? Ni kwa sababu ya msimamo huo wa Mwalimu Nyerere, Afrika Kusini ilijitoa kwenye umoja huo kama jamhuri. Ndipo Tanganyika iliingia rasmi. Ilihitaji uthubutu na kujiamini kutamka kisha kusimamia kilichotamkwa. Utaona kuwa Taifa lilipata upendeleo mkubwa kuwa na kiongozi kama Mwalimu Nyerere.

Misimamo hiyo ndiyo zao la tamko la kupeleka matumaini kwa waliokata tamaa. Wazimbabwe wakaonyeshwa na Tanzania kuwa japo wanapitia nyakati ngumu, lakini angalau walikuwa na ndugu zao Watanzania, waliokuwa tayari kuwapigania kwa hali na mali. Wazimbabwe wakaishi Tanzania wakiweka kambi ya maandalizi ya kuikomboa nchi yao.

Ni Zimbabwe iliyomfanya Mwalimu kutishia kuiondoa Tanzania Jumuiya ya Madola kwa sababu vitendo vya Waingereza kwa Wazimbabwe.

Ukiulizwa swali Mwalimu Nyerere ni nani, jibu ni lilelile, Baba wa Taifa. Miaka 20 tangu kifo chake, imebaki hivyo na haitabadilika kamwe.

Advertisement