MAONI: Tumuenzi Mwalimu Nyerere na falsafa ya elimu ya kujitegemea

Imepita miaka 21 sasa tangu kutokea kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius  Nyerere alipoliacha taifa katika mikono ya Watanzania likiwa taifa salama . Ingawa hayupo nasi kimwili lakini kiroho na kifikra yupo nasi,  
kwa kuwa mawazo ya Nyerere na falsafa zake bado zinaishi katika kila kichwa cha Mtanzania mwenye fikra za kizalendo na mapenzi mema kwa nchi yake.

Ikumbukwe Nyerere alibadilisha fikra zake kuwa vitu halisi vinavyoonekana, aliyatoa mawazo kichwani na kuyaweka katika utendaji na kupata matokeo na moja ya mawazo na fikra zake ambazo alitamani kuziona katika taifa na Afrika ni elimu inayolingana na uhitaji wa jamii na Tanzania, elimu ya kujitegemea na kwake hii ndio ilikuwa elimu bora.

Elimu ya kujitegemea ni mawazo juu ya mfumo wa elimu ambayo iliendana na uhalisia wa jamii iliyokuwapo wakati na baada ya uhuru kwa kuwa aliamini elimu hii ingekuwa ufunguo wa ujenzi wa jamii mpya ya Watanzania waliotoka katika mikono ya ukoloni, waletwe pamoja kupitia sera vijiji vya ujamaa kisha wale watakaopata elimu hii walete mabadiliko kwa kuwekeza na kuijenga jamii. 

Yeye aliamini elimu hii au mfumo wowote wa elimu yenye manufaa ilipaswa kuwa na sifa nyingi ikiwemo; Elimu ni lazima iitumikie jamii, wakati Serikali, wazazi na jamii ikitumia fedha na rasilimali nyingi kwa ajili ya kusomesha, lilikuwa ni deni kubwa kwa wasomi hao na ilikuwa ni lazima waje walilipe kwa kuitumikia jamii na si vinginevyo. 

Nyerere alikuwa na maana kuwa hakuna msomi ambaye angepata elimu halafu imfaidishe yeye binafsi baada ya serikali na jamii kumgharamikia. Imani hii ya Nyerere dhidi ya elimu aliyotamani imebaki miongoni mwetu lakini matokeo yake ni madogo kutokana na misingi ya elimu yenyewe kutokuwapo tena katika mfumo wa elimu wa sasa. 

Mfano, licha Serikali, wazazi, walezi na jamii kusomesha vijana wengi, baada ya kuhitimu wengi wa wasomi hawa huishia kusikojulikana, wengi wao hurudi katika jamii na kuwa mizigo katika familia badala ya kuwa suluhisho katika jamii. 

Dhana hii ya wasomi kuwa na deni la kuitumikia jamii, si sawa kila mwaka taifa kutoa maelfu ya wasomi katika vyuo, taasisi na shule halafu wanakaa tu bila kufanya chochote jamii isinufaike.

Ni lazima wasomi wawe sehemu ya jamii, kuchangamana na kutangamana na jamii iliyomkuza na kumsomesha msomi ndio ilikuwa shabaha ya na misingi ya elimu ile aliyoiamini Mwalimu Nyerere.

Katika nukuu zake aliwahi kusema kuwa watu walioelelimika wanaweza kuwa na faida wakiwa ni sehemu na wanajamii kwelikweli, wanaojaribu kuibadilisha, wanaokuwa na jamii katika hali mbaya na nzuri, kujitoa kikamilifu kwa kila kinachotokea.

Alikuwa na fikra njema sana lakini ikiwa imepita miaka 21 tangu atutoke, asilimia kubwa ya wasomi hivi sasa hawataki kuwa sehemu ya jamii. Wasomi wa leo wakishapata elimu na maarifa kupitia serikali na jamii, wanajitenga, wamejiweka kwenye tabaka lao peke yao. 
Dhumuni kuu la mtu kutafuta elimu ni kupata maarifa ili yawe suluhisho la matatizo yanayoikabili jamii.

Mfano watu wanasomea uuguzi ili wawe suluhisho la maradhi, wanasome uhandisi ili wawe suluhisho la ujenzi wa makazi na namna nyingine ya ujenzi na taaluma nyingine nyingi. 

Jamii yeyote yenye wasomi halafu haiwezi kutoa suluhisho la tatizo lolote inajidanganya kuwa ina wasomi na hawakuwa na sababu yoyote ya kusoma.

Kama taifa lina wasomi lakini haliwezi hata kutoa mawazo kama sehemu ya suluhisho ya jambo linaloikabili jamii, ni sawa na hakuna wasomi. 
Vilevile viongozi wengi wa mataifa ya Afrika wamekuwa si wazalendo kwa watu wao, wanaahidi mazingira ya fursa za kazi kwa watu wao lakini hawatimizi, wanaimba kuhusu vijana kujiajiri huku wao wameajiriwa na wanaogopa kufukuzwa kazi. 

Katika miaka 21 ya kifo cha Simba wa Afrika, mzalendo, tunapaswa kuutazama upya mfumo wa elimu kama una sifa alizotamani kuziona Nyerere au la. Huko ndiko kumuenzi kwelikweli.

Amani Njoka ni Mwandishi wa habari wa Mwananchi. 0672395558