MPYA: Mgonjwa wa corona agundulika nchini Tanzania

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Ugonjwa wa Virusi vya Corona (CODIV-19) ulioanzia nchini China na kusambaa mataifa mbalimbali dunia, leo Jumatatu umethibitishwa na Serikali ya Tanzania kuwapo kwa mgonjwa mmoja raia wa nchi hiyo aliyetokea Ubelgiji.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania amethibitisha kupatikana kwa raia mmoja wa nchi hiyo mwenye ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 16, 2020, Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema mgonjwa huyo mwanamke mwenye umri wa miaka 46 aliwasili Tanzania jana Jumapili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Ubelgiji.

Waziri Ummy amesema mgonjwa huyo ambaye ni Mtanzania alikaguliwa uwanja wa ndege lakini hakugundulika kuwa na ugonjwa huo lakini baadaye alianza kujisikia vibaya alipofika hotelini.

“Kwa mujibu wa maelezo yake, alianza kujisikia vibaya alipofika hotelini ndipo alipoamua kujitenga na watu kisha akaenda hospitali,” amesema Waziri Ummy

“Sampuli za vipimo vyake zilikuja Dar es Salaam na imethibitika kuwa na virusi vya Corona. Niwasihi Watanzania watulie tunachukua hatua kuthibiti,” amesema

“Tunaweza kudhibiti huu ugonjwa endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake. Niviombe vyombo vya habari visitoe taarifa za kuwashtua watu, Serikali tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara,” amesema