Breaking News

MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Nyerere atangaza Baraza la Mawaziri wa Muungano -15

Wednesday April 24 2019

 

By William Shao

Baada ya sherehe fupi ya kuurasimisha Muungano, siku iliyofuata yaani Aprili 27, Rais wa Tanzania, Julius Nyerere alitangaza baraza lililokuwa na mawaziri 23, huku watano wakitokea Zanzibar.

Said Msawanya aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Misitu na Wanyama Pori; Jeremia Kasambala (Biashara na Ushirika), Paul Bomani (Fedha), Oscar Kambona (Mambo ya Nje), Rashidi Kawawa (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), na Tewa Said Tewa (Ardhi, Makazi na Maji).

Wengine ni Job Lusinde (Mambo ya Ndani), Kassim Hanga (Viwanda, Madini na Nishati), Solomoni Eliufoo (Elimu), Dereck Bryceson (Afya), Michael Kamaliza (Kazi), Sheikh Amri Abeid (Jamii na Maendeleo ya Utamaduni), Austin Shaba (Serikali za Mitaa na Nyumba), Hassan Moyo (Sheria) na Abdul Idris Wakil (Habari na Utalii).

Baada ya Nyerere kutangaza baraza lake la mawaziri, Balozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, William Leonhart, alituma taarifa ya kilichofanyika.

“Sina shaka kwamba Watanganyika wanatazamia kwamba Serikali ya Zanzibar itapunguza au kuziondoa kabisa nguvu za kikomunisti kwa kutumia siasa za kutofungamana na upande wowote, hasa ikizingatiwa nguvu na kasi ambayo Wakomunisti wanayo huko Zanzibar,” aliandika katika ujumbe huo.

“Ni dhahiri kwamba wataukubali Muungano na wala hawatajaribu kuifanyia vitisho Serikali ya Muungano. Naamini ni muhimu kwa Nyerere kupewa msaada wa hali ya juu kutoka (nchi za) Magharibi kuanzia hapa mwanzoni.”

Advertisement

Siku mbili baadaye, aliyekuwa balozi mdogo wa Marekani visiwani, Frank Carlucci alituma ujumbe kuelezea kuwa hali ya mambo inaonekana kuwa ya kawaida kisiwani Unguja na kwamba anaona ni mapema mno kwa Waingereza kuingilia.

“Naamini kwamba ni lazima tumpe (Mwalimu) Nyerere msaada na kumwachia yeye mwenyewe aendeshe mambo isipokuwa tutakapokuwa tu na hakika kwamba mambo yanamshinda ndipo tuingilie kati. Kwa sasa anaonekana kuyaweza mambo,” aliandika Carlucci

Awali ilisemekana kuwa kabla ya siku ya Muungano, CIA ilituma taarifa kutaka iwepo tahadhari dhidi ya Abdulrahman Babu na Ali Mahfudhi kwa hofu kuwa wangeweza kufanya lolote usiku wa Aprili 26.

Abeid Karume

Advertisement