MUUNGANO TANGANYIKA -ZANZIBAR 1964: Kuzaliwa OAU na ndoto ya Afrika moja (1)

Muktasari:

Miaka 55 iliyopita Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuwa nchi moja inayojulikana kama Tanzania. Kumekuwepo na maswali mengi kuhusu chanzo cha muungano huo na kuibuka kwa wazo hilo. Je, Mwalimu Julius Nyerere alilipataje wazo la kuziunganisha nchi hizo? Kwanini ilikuwa ni lazima Tanganyika na Zanzibar ziungane? Nchi hizi zingekuwaje kama hazingeungana? Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni dhahiri kiasi gani? Watafiti, wachambuzi na waandishi tofauti wameandika kuhusu utata wa kuibuka kwa muungano. Mwandishi wetu, William Shao anachambua taarifa tofauti kuhusu chanzo cha muungano. Fuatana naye katika mfululizo wa makala haya kuhusu Muungano inayoanza na jinsi viongozi wa kwanza Afrika walivyoona umuhumu wa bara hili kuwa na sauti moja.

Usiku wa kuamkia Januari 12, 1964 ambayo ilikuwa Jumapili, kulitokea mapinduzi yaliouondoa madarakani utawala wa kisultani visiwani Zanzibar. Mapinduzi hayo ni sehemu ya mlolongo wa mambo yaliyosababisha maasi ya jeshi nchini Tanganyika yaliyofanyika juma moja tu baadaye—yaani usiku wa kuamkia Jumapili ya Januari 19, 1964—na takriban siku 100 baadaye Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuwa Tanzania.

Kwa kuzingatia yale yaliyotokea Zanzibar Januari 12, 1964, yakijumlishwa na yaliyotokea Tanganyika Januari 19, pamoja na athari kwa nchi zote mbili za Tanganyika na Zanzibar, mawazo ya Muungano wa nchi hizo yalizaliwa katika kipindi hicho cha matukio makubwa cha robo ya kwanza ya mwaka 1964.

Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa unaitwa AU, ulianzishwa Mei 25, 1963, ikiwa ni miezi 11 kabla ya Muungano.

Katika mkutano wa kuanzisha OAU uliofanyika ukumbi wa Addis Ababa Africa nchini Ethiopia, Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere, alisema: “Katika maafikiano yetu haya, hata mpaka ukombozi wa mwisho wa bara letu la Afrika, tumekubaliana wote kwa kauli moja wakati wa kutumia maneno matupu umepita. Huu ni wakati wa vitendo.

“Wakati wa kuwatazama ndugu zetu wakipambana umepita, wakati umefika kuanzia sasa na kuendelea kwa Umoja wa Afrika kuwasaidia ndugu zetu wanaopambana waweze kuwa huru.”

Pengine katika moyo huo, Nyerere alisaidia vyama na vikundi vingi vya ukombozi vya kusini mwa Afrika, kama Frelimo ya Msumbiji na ANC ya Afrika Kusini.

Katika mkutano huo, viongozi walitaka nchi za Afrika ziungane kuwa nchi moja.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, kiongozi wa Ethiopia, Haile Selassie (71), alielezea umuhimu wa kuwa na sauti moja.

“Pamoja na juhudi zetu za miaka yote iliyopita, tulichokuwa tumekosa kabisa ni nguvu ya kutuwezesha tuzungumze kwa sauti zetu wenyewe kila tunapotaka kusema au kufanya uamuzi wa maana tunapohitaji kuamua mambo yetu,” alisema.

“Lakini leo tumepata chombo kitakachotuwezesha kuzungumza kwa sauti zetu wenyewe kila tunapotaka kusema na kufanya uamuzi wetu kila tunapotaka kufanya. Natumaini chombo hiki kitakuwa msimamizi wa kweli kwa matumaini na matatizo yetu.”

Baada ya Selassie kuzungumza, alifuata Kwame Nkrumah, rais wa Ghana.

“OAU ni chombo kilicho juu zaidi kuliko dola ya nchi yoyote. Ni chombo kinachoweza kupatikana kwa njia za kisiasa. Yapasa kitunzwe,” alisema Rais Nkrumah.

“Maendeleo ya kisiasa na ya kijamii katika bara la Afrika yatapatikana kupitia chombo hiki. Hakuna njia nyingine itakayoliwezesha bara la Afrika kupata mambo hayo. Tukiondoka hapa (Addis Ababa) turudi kwa wananchi wa Afrika na jambo la kuwaambia. Ahadi tunazotoa leo hapa, za kulikomboa bara la Afrika, tuhakikishe zinatimia.

“Kwa hiyo sasa tujivunie kuwa haturudi kwa wananchi wetu mikono mitupu, bali tunarudi na Azimio la Nchi Huru za Afrika, na tuwe na matumaini kuwa Umoja wa Afrika utadumu daima, ... na huu ni mwanzo wa muungano wa bara lote la Afrika kuwa nchi moja.”

Waziri Mkuu wa Nigeria, Abubakar Tafawa Balewa alizungumzia umuhimu wa maeneo ya kukubaliana. “Msimamo wa Nigeria ni kwamba, kama tunautaka Umoja huu wa Afrika udumu, ni lazima tukubaliane katika mambo ya msingi,” alisema.

“Kwanza, mataifa ya Afrika ni lazima yaheshimiane na yote yakubaliane kuwa kukandamizwa kwa taifa moja la Afrika ni sawasawa na kukandamizwa kwa mataifa yote ya Afrika. Hata kama taifa linalohusika ni dogo kadiri gani, yote yana dola lake.”

Kiongozi wa Algeria, Ben Bella, naye alitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo mambo wanayokubaliana.

“Tusiuache Umoja wa Afrika uwe wa maneno matupu. Tutakuwa tumepoteza wakati wetu na matumaini ya watu wetu ikiwa tulichoazimia leo ni maneno matupu,” alisema.

Ndipo Nyerere aliposimama na kuongeza uzito katika hoja hiyo.

“Katika maafikiano yetu haya, hata mpaka ukombozi wa mwisho wa bara letu la Afrika, tumekubaliana wote kwa kauli moja kuwa wakati wa kutumia maneno matupu umepita. Huu ni wakati wa vitendo,” alisema.

“Wakati wa kuwatazama ndugu zetu wakipambana umepita. Wakati umefika kuanzia sasa na kuendelea kwa Umoja wa Afrika kuwasaidia ndugu zetu wanaopambana waweze kuwa huru.”

Ingawa Kwame Nkrumah alisisitiza sana kuunganishwa kwa nchi zote za Afrika ili iwe nchi moja, hadi alipopinduliwa 1966 hakuwa ameunganisha hata nchi moja. Jumanne ya Februari 21, 1966, Nkrumah alikwenda Hanoi kupitia India, Pakistan na Burma, lakini nyuma yake serikali yake ikapinduliwa.

Miezi 11 baada ya kuanzishwa kwa OAU, Tanganyika iliungana na Zanzibar. Ni kweli kwamba viongozi wa Kiafrika waliokutana Addis Ababa walitaka nchi za Afrika ziungane, ili Afrika iwe nchi moja, lakini je, kuungana huko ni matokeo ya rai hizo?

Itaendelea kesho