Maalim Seif aomboleza kifo cha Sultan Qaboos

Monday January 13 2020

 

By Muhammed Khamis, Mwananchi [email protected]

Unguja. Mshauri mkuu wa Chama ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kufariki kwa mfalme wa Oman Sultan Qaboos bin Said kumeacha pengo kubwa kwa nchi hio pamoja na mataifa mengi ulimwenguni.

Maalim Seif ameyasema hayo leo Januari 13 wakati alipofika ubalozi mdogo wa Oman uliopo Migombani mjini Unguja.

Amesema kwa miaka mingi Zanzibar na Omar zimekua na ukaribu wa kindugu jambo ambalo linapaswa kutunzwa na kuenziwa.

Amesema kuwa wananchi wa Zanzibar kwa namna moja au nyingine wameguswa na msiba huo na wapo pamoja na wenzao wa Oman katika kumuombea marehemu.

Sambamba na hilo Maalim Seif amesema Taifa la Oman limepoteza mtu muhimu sana aliyejaaliwa na busara katika kipindi chote cha uongozi wake.

Maalim Seif pia amesema kuwa anaamini mrithi wa kiti hicho cha ufalme wa Oman atayaendeleza yale yote yalioasisiwa na mtangulizi wake ikiwemo mashirikiano bora na Zanzibar pamoja na Tanzania kwa ujumla.

Advertisement

Kwa upande wake balozi mdogo wa Oman visiwani hapa,  Dk Ahmed Hamood A-habs alisema kwa niaba ya watu wa Oman amepokea salam hizo za pole na kwamba zitawafanya wawe wenye kufarijika.

Sultan Qaboos alifariki dunia Januari 10 mwaka huu akiwa ameliongoza taifa hilo tangu mwaka 1970 akichukua madaraka kutoka kwa baba yake, Said bin Taimur.

Advertisement