Maalim Seif awa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Wajumbe wa mkutano mkuu wa pili wa ACT- Wazalendo wamemchagua Maalim Seif kuwa mwenyekiti wa chama hicho huku Zitto Kabwe akitetea nafasi yake kiongozi wa chama kwa mara nyingine.

Dar es Salaam.  Maalim Seif amechaguliwa kuwa mwenyekti mpya wa chama cha ACT- Wazalendo huku Zitto Kabwe akitetea nafasi kiongozi wa chama hicho kwa mara ya pili mfululizo katika uchaguzi uliofanyika jana Machi 14, 2020.

Kwa matokeo hayo Maalim Seif ambaye pia ni mshauri mkuu wa ACT-  Wazalendo anakuwa mwenyekiti wa pili wa chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014.

Maalim Seif na Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini walichaguliwa usiku wa kuamkia leo Jumapili Machi 15, 2020 katika mkutano mkuu wa pili wa chama hicho uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi wa viongozi wa nafasi ya uenyekiti na kiongozi wa ACT- Wazalendo.

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi wa chama hicho, Omar Said Shabaan amesema jumla wajumbe walioshiriki mchakato huo ni 375, kura halali zilikuwa 367 na zilizoharibika nane.

" Zitto Kabwe amepata kura 276 sawa na asilimia 73.6 wakati Ismail Jussa amepata kura 91 sawa na asilimia 24.2.Maalim Seif amepata kura 337 sawa na asilimia 93.30 dhidi ya wapinzani wake," amesema

Huku akikatizwakatizwa na kelele za wajumbe wa mkutano huo waliokuwa na shauku ya kutaka kujua matokeo hayo, Shabaan amesema Maalim Seif aliwashinda Nyangaki Shilungushela aliyepata kura nne sawa asilimia 1.10 na Yeremia Maganja kura 20 sawa asilimia 5.55.

"Kwa matokeo haya nikiwa mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi namtangaza kwenu Maalim Seif kuwa mwenyekiti wa ACT -Wazalendo," amesema Shabaan

Baada ya kutangazwa kwa matokeo ukumbi huo ulilipuka kwa shangwe na vigelegele kwa wajumbe kushangalia baada ya mchakato huo kukamilika usiku wa kuamkia leo Jumapili.

Uchaguzi huo unaendelea leo katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya umakamu uenyekiti wa Zanzibar na Tanzania bara ambao unatajwa kuwa na mchuano mkali, kisha kesho nafasi ya katibu mkuu.