Maaskofu Katoliki Tanzania kuratibu mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere Mtakatifu

What you need to know:

  • Mchakato wa kumtangaza Mwalimu Julius Nyerere kuwa Mtakatifu ulianzishwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Musoma mkoani Mara ukiongozwa na aliyekuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo, Justin Samba ambaye sasa ni marehemu.
  • Mwalimu Nyerere alizaliwa Kijiji cha Mwitongo, Butiama mkoani Mara Aprili 13, 1922, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 akiwa London nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu

Butiama. Mchakato wa kumtangaza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa Mtakatifu ulioanzishwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Musoma mkoani Mara nchini Tanzania umehamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 wakati wa ibada maalum ya kumwombea Mwalimu Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Butiama, Padre Daniel Inc amesema uratibu wa mchakato huo umehamishiwa chini ya Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC).

"Kwa kigezo kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa Kitaifa mchakato wa kumkangaza kuwa Mtakatifu sasa utasimamiwa na Baraza la Maaskofu badala Jimbo Kuu la Musoma kama ilivyokuwa awali," amesema Padre Inc

Kuhusu kuhamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre Inc amesema "Kutokana na Mwalimu Nyerere kuishi na kusali Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa kipindi kirefu, mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu pia umehamishiwa huko."

Amewasihi waumini wa Kanisa Katoliki kufanya maombi kwa ajili ya Mwalimu Nyerere na kutangaza miujiza inayotokea wakati wa maombi hayo kama njia ya kufanikisha mchakato wa kumtangaza mwasisi huyo wa Taifa kuwa Mtakatifu.