Mabadiliko ya teknolojia yanalitesa Shirika la Umeme Tanzania

Muktasari:

Tanesco yasema mabadiliko ya Teknolojia yanachangia vifaa kubakia bohari bila kuuzwa.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya teknolojia yametajwa kuwa sababu kuu ya kuchangia vifaa vingi vinavyonunuliwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kubakia katika bohari kwa kukosa matumizi na kusababishia shirika kupata hasara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Alexander Kyaruzi amesema hayo leo Ijumaa Februari 14, 2020 alipotembelea bohari ya Kurasini iliyoko Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti huyo na timu yake wamefika kwenye bohari hiyo kukagua vifaa vilivyonunuliwa kwa matumizi mbalimbali na kukuta baadhi vikiwa muda wake wa matumizi ushaisha na haviitajiki sokoni.

“Tanesco inajitahidi kukusanya mapato na matumizi na bohari inakusanya fedha nyingi sana, ndiyo maana tumekuja hapa kama bodi ya wakurugenzi kuona kama kuna njia ya kupunguza matumizi kwa shirika letu,” amesema Kyaruzi.

Amesema baada ya ukaguzi, wamebaini kuna vifaa vingine viliagizwa vingi na kama vingenunuliwa ndani ya muda, visingeweza kupitwa na wakati.

Hivyo amesema uongozi wa Shirika unapotaka kuagiza vifaa kuanzia sasa,  viwe vya matumizi ya mwaka mmoja au isizidi mitatu.

Kyaruzi ambaye ameteuliwa kwa mara ya pili Rais wa Tanzania, John Magufuli kuongoza bodi hiyo, amesema  wanajivunia hali ya sasa ambayo inaifanya Tanesco isijiendeshe kwa hasara.

“Wakati naanza awamu ya kwanza Mei, 2016 nilipoteuliwa, nilikuta shirika linatengeza hasara ya Sh300 bilioni na sasa zinapungua mwaka hadi mwaka baada ya kuongeza mapato na kupunguza matumizi,” amesema mwenyekiti huyo wa bodi.

Amesema Tanesco ambayo awali ilikuwa inategemea ruzuku ya uendeshaji kutoka serikali kuu, hivi sasa inatumia faida wanayopata kujiendesha.

Kyaruzi amesema jambo la pili wanalojivunia ni upatikanaji wa umeme kwa wananchi kwa kiwango cha juu.

“Tuna miradi mingi ya kusafirisha umeme ukiwamo wa kutoka Singinda wa Kilovoti 400 tunaupeleka Manyara, Arusha na utaenda hadi Namanga na tutajiunga na Kenya, tunaweza kuuza Uganda au Ethiopia pia,” amesema Kyaruzi.

Awali, wajumbe wengine wa bodi, walihoji namna ya utunzaji wa vifaa hivyo, ununuzi na utunzaji wa rekodi zinazokuwepo baada ya kuuza pamoja na kutumia mfumo wa kisasa wa kidigitali ili kujua kama Tanesco inafaidika.

Hata hivyo, ofisa Bohari Mkuu wa Tanesco, Emmanuel Mwasandube alitaja changamoto ya kukosa ghala la kisasa la kuhifadhia mitambo na vifaa vya umeme katika bohari ya Kurasini.

Amesema hali hiyo imesababisha waweka vifaa vingi kwenye eneo la wazi ambako vinanyeshewa mvua na kupata kutu.

Amesema hata vile vinavyotakiwa kuhifadhiwa kwenye mbao maalumu, nazo zimekuwa zikioza na kusababisha vifaa kuwekwa chini.

“Tukipata ghala la kisasa au kuziba kwa juu itakuwa vizuri zaidi,” amesema Mwasandube.

Amesema Tanesco imejiimarisha kwenye ukusanyaji wa mapato kutokana na kuuza vifaa mbalimbali kwa wateja na wadau na kumbukumbu zake kuwekwa kwenye mfumo maalumu.