Madereva, makondakta waandaliwa mtihani

Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe akizindua sare mpya kwaajili ya madereva na makondakta wa dalada Mkoa wa Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) imeanzisha mfumo mpya ambao madereva wote wa magari ya abiria watatakiwa kufanya mtihani na kupewa vyeti pamoja na kuwasajili mkondakta.
Akizungumza leo Jumatatu Aprili 6,2020 wakati wa uzinduzi wa sare mpya za madereva na makondakta Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilano, Isack Kamwelwe amesema kanuni hizo zinalenga kuifanya kazi ya udereva kuwa taaLuma inayoheshimika.
“Kupitia kanuni zilizotangazwa za udahili wa madereva na usajili wa makondakta madereva wa magari ya abiria watatakiwa kufanya mtihani na kupatiwa vyeti na Latra,”amesema Kamwelwe
“Uvaaji wa sare safi na nadhifu utakuwa ni sehemu ya kuwafanya nadereva wetu watambulike na kuheshimika,” amesema.

“Wakati mwingine kazi ya udereva imekuwa haishimiki kutokana na madereva wenyewe kutovaa nguo nzuri, safi na nadhifu sare nzuri mlizochagua wenyewe zitawafanya kazi yenu iheshimike.”
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliad Ngewe amesema uvaaji wa sare kwa madereva na makondakta uko kisheria ambapo wamiliki huzinunua na kuwapa wafanyakazi wao.
“Viongozi mbalimbali wa vyama pamoja na wamiliki walikaa pamoja na kuamua kubadilisha rangi kutoka kaki na kuwa zambarao kwa lengo la kubadilisha muonekano wa watoa huduma,”amesema Ngewe
Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam, Kismat Jaffar amesema sare zilizokuwa zinatumika zikivaliwa mara mbili haifai au kupauka inapofuliwa.
“Kwa kushirikiana na wadau wa usafiri tulikubaliana kubadilisha sare na kuwa na sare zenye ubora kutoka rangi ya kaki na kuwa zambarau,”amesema Kismat
Kaimu Katibu wa Darcoboa, Shifwaya Lema amesema utaratibu wa uvaaji wa sare hizo utabadilika kidogo ambapo Jumatatu hadi Alhamisi yatavaliwa mashati na Ijumaa hadi Jumapili zitakuwa ni siku za kuvaa tisheti.