Madiwani 11 wa Chadema Mbeya wahama CCM, Dk Bashiru amtumia salamu Sugu

Muktasari:

  • Katibu wa Mkuu wa CCM,  Dk Bashiru Ally amewapokea madiwani 11 Chadema katika Jiji la Mbeya huku akimtumia salamu mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu kuwa ameshaanza kufunga mitambo.

Dodoma. Madiwani 11 wa Chadema Jiji la Mbeya wakiongozwa na meya wa Jiji hilo,  mchungaji David Mwashilindi wamehama Chadema na kujiunga na CCM.

Kati ya madiwani hao, 10 ni wa kuchaguliwa kutokana kata mbalimbali na mmoja alikuwa wa viti maalumu ambao kwa pamoja wanasema wamekimbia magomvi katika chama chao cha awali.

Leo Jumatatu Februari 24, 2020, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma aliwapokea madiwani hao akisema bado kuna kundi kubwa ambalo linakuja nyuma kutoka katika mikoa mbalimbali.

Dk Bashiru alitumia nafasi hiyo kumtumia salamu mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu kwamba alimuahidi angewasha moto sasa kazi imeanza.

Katibu huyo amesema Sugu ni rafiki yake na kuwa alimuahidi angefunga mitambo, sasa kazi imekwishaanza na kuwa atakwenda Mbeya mapema kabla ya joto halijapoa ili akafunge kazi huko.

“Lakini naomba mje na mbinu, mikakati na siri mlizotumia huko, sisi tunawakaribisha na uzuri wa chama chetu hakuna mwanachama wa siku nyingi wala mpya, wote wana haki sawa ila kinachoangaliwa ni miiko na maadili, naomba mkajiunge kwenye matawi yenu ya CCM huko,” amesema Dk Bashiru.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, aliyekuwa Meya Mchungaji David Mwashilindi amesema walichokimbia Chadema ni magomvi ya kila siku ambayo yanafanya mipango ya maendeleo kufeli.

Mwashilindi amesema wamehama kwa hiyari yao na wameingia CCM na idadi ya wapiga kura pamoja na mbinu kubwa ambazo amesema watazitumia kwa ajili ya kukisaidia chama hicho tawala, akisema wako nyumbani sasa.