Madiwani wanane CUF wahamia CCM, wamtaja Magufuli

Wednesday January 15 2020

 

By Burhani Yakub, Mwananchi byakub @mwananchi.co.tz

Tanga. Ngome ya Chama cha Wananchi (CUF) katika Jiji la Tanga imetikiswa baada ya madiwani wanane wa chama hicho kati ya 13 kujiuzulu na kuhamia CCM.

Wakiongozwa na aliyekuwa naibu Meya, Mohamed Haniu wametangaza kuhamia CCM leo Jumatano Januari 15, 2020 na kupokewa na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Madiwani hao ni Mswahili Njama (Chongoleani), Said Alei (Masiwani), Nassoro Mohamed (Tongoni), Habib Mpa (Ngamiani kati), Hidaya Ahmed, Sureha Mahadhi na Mwanasha Abdallah (wote Viti maalum)

Mwingine aliyejiunga CCM ni Hidaya Ahmed ambaye alikuwa mwanachama maarufu wa CUF mjini Tanga.

“Tumejiunga CCM kwa sababu yale tuliyokuwa tunayapigia kelele tukiwa CUF yanatekelezwa na Rais John Magufuli. Hatuoni sababu ya kuendelea kubaki huko,” amesema Haniu alipoulizwa sababu za kuhamia CCM.

Akizungumza baada ya kuwapokea madiwani hao, Dk Bashiru amesema mwanachama anayejiunga CCM leo ana haki sawa na mwanachama wa muda mrefu wa chama hicho tawala nchini Tanzania.

Advertisement

Dk Bashiru amesema madiwani hao kujiunga CCM ni sehemu ya kazi aliyoanza kuifanya katika ziara yake iliyoanza Zanzibar.

Advertisement