Maendeleo endelevu yanahitaji Tehama

Muktasari:

Wakati utawala wa Dijitali ukiendelea kushika hatamu, Makamu wa rais wa kampuni ya Huawei kwa ukanda wa kusini mwa Afrika David Chen amesema Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) imetajwa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja kwa moja na maendeleo endelevu

Dar es Salaam. Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imetajwa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo endelevu ikiwamo huduma bora za elimu, afya, viwanda, ubunifu, miundombinu na usawa wa kijinsia.

Hayo yameelezwa na Makamu wa rais wa kampuni ya Huawei kwa ukanda wa kusini mwa Afrika, David Chen ambaye yupo hapa jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa Tehama wa Jumuiya za maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (Sadc).

“Matumizi ya dijitali kwa wote yanahitaji ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya umma pamoja na asasi za kiraia, Serikali inapaswa kutumia nafasi yake katika suala la sera kwa kuweka mazingira ambayo yanafanya huduma za dijitali kupatikana kwa bei nafuu,” alisema Chen.

Aidha kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia inaonyesha asilimia 47 tu ya watu dunia ndiyo hutumia mtandao wa internet na wengi wao wako Afrika, hata hivyo takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha takribani asilimia 50 ya Watanzania hutumia huduma hiyo.

Hata hivyo, wataalamu wa Tehama wanasema ubunifu katika huduma na mambo yanayoleta suluhisho ni muhimu kwa manufaa ya bara la Afrika kutokana na ongezeko la matumizi ya mtandao wa 4G na 5G inayotarajiwa.