VIDEO: Mafuriko yaivuruga Rufiji

Thursday March 26 2020

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha mafuriko na kukata mawasiliano ya ndani wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na kuziacha zaidi ya kaya 350 bila makazi.

Mafuriko hayo yameharibu barabara mbalimbali za wilaya hiyo ikiwamo inayotoka Kibiti kwenda katika eneo la mradi wa umeme (MW 2,115) katika maporomoko ya Mto Rufiji ambako magari yenye vifaa yamekwama ndani ya maji.

Pia, baadhi ya barabara zinazounganisha kata 13 za Rufiji hazipitiki kutokana na makaravati kusombwa na maji na Daraja la Ikwiriri limeonyesha dalili za kubomoka, hali inayotishia kukatika kwa mawasiliano na mikoa ya kusini.

Akizungumzia suala hilo, mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alisema msaada unaohitajika haraka kwa sasa ni wa chakula na mbegu ili kuwawezesha wakulima kupanda mazao ya muda mfupi ili kuepuka njaa inayoweza kuwakumba.

Alisema baada ya mafuriko hayo, kaya hizo zilihamishiwa katika Shule ya Msingi Mhoro na majengo ya Serikali ya Chumvi, lakini baadaye eneo hilo pia likajaa maji huku kukiwa na tatizo la chakula, hivyo wananchi hao wakaombwa kwenda kwa ndugu na jamaa zao.

“Pale tulishindwa kuwahudumia kwa kuwa chakula na mahitaji mengine havikuwapo ndipo tukawaomba watafute sehemu pa kwenda, yaani hatujui wanaishi wapi kwa sasa,” alisema Mchengerwa.

Advertisement

“Sisi wananchi wa Rufiji hatuhitaji vyakula vya msaada nyakati hizi za kilimo kwa kuwa tuna uwezo wa kulima, lakini vyakula vyetu tulivyolima na kuvuna hatuwezi kuvipata tena, vimeondoka na maji,” alisema mbunge huyo.

“Hivyo tunaomba msaada wa chakula na mbegu tulime tena.”

Alisema asilimia 99 ya wananchi wa jimbo hilo lenye watu zaidi ya laki tatu wanategemea kilimo na asilimia moja wanaotegemea ufugaji, mifugo yao imekufa kutokana na mafuriko.

Mbunge huyo aliiomba Serikali kuwapa misaada mbalimbali wananchi wake kwa sababu hawana huduma zozote na ili watoke eneo moja kwenda jingine wanahitaji kupanda boti au mitumbwi ambayo gharama yake ni Sh5,000, kiwango ambacho alisema hawawezi kukimudu.

Mchengerwa alitahadharisha kuwa mafuriko hayo yanaweza kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya mikoa ya Kusini na Pwani kutokana na Daraja la Ikwiriri kuanza kuliwa na maji pembeni na nguzo zimeanza kutoka.

“Kukatika kwa daraja hilo kutamaanisha kwamba magari yanayotoka Dar es Salaam hayataweza kwenda mikoa ya kusini na yale yanayotokea kusini hayataweza kupita,” alisema Mchengerwa

Mkurugenzi wa Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe alisema baada ya kupokea taarifa za mafuriko hayo amefika Rufiji na kutoa msaada wa boti mbili na wazamiaji ili kuwaokoa wananchi waliokuwa wamezingirwa na maji.

Alisema boti hizo zitafanya kazi katika vijiji 13 vilivyoathirika, tisa vya Mhoro na vingine vya Chumvi.

Kanali Matamwe alisema ametoa maelekezo kwa kamati ya maafa ya wilaya kujipanga vizuri kwa kuwa eneo hilo linapokea maji kutoka mikoa ya Singida na Iringa ambako mabwawa ya Mtera na Kidatu yamejaa.

Ujenzi Bwawa la Nyerere

Kuhusu mradi wa umeme unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115 katika Mto Rufiji, Mchengerwa alisema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa barabara inayokwenda eneo hilo.

Alisema barabara hiyo ya kilomita 150 inayoanzia Kibiti hadi eneo la mradi, imeharibika na magari mengi yaliyobeba vifaa mbalimbali vya ujenzi kama saruji, mabomba na chuma yamekwama.

Hali hiyo, mbunge huyo anasema, inatishia kumalizika mapema kwa mradi huo uliopangwa kumalizika ndani ya miezi 36 kwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vifaa vinavyopelekwa katika mradi vinategemea barabara hiyo.

“Kwa bahati mbaya wasaidizi wa Rais hawamwambii ukweli,” alisema.

“Kama wangemwambia ukweli mkandarasi anayejenga mradi huu, angeanza kuboresha barabara kwanza lakini kwa sababu hawakumwambia ukweli, walimwambia vifaa vinapitia Morogoro.”

Alisema siku ya uzinduzi wa mradi, alitarajia angepewa nafasi ya kuzungumza lakini ilishindikana.

“Kama ningezungumza, ningesema ukweli kuhusu vifaa. Ukisema vifaa vitoke Mtwara vikapite Morogoro ni umbali zaidi ya mara tatu,” alisema mbunge huyo.

Mchengerwa, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema jukumu la kuboresha miundombinu kuelekea katika mradi ni la mkandarasi na anaposema atakamilisha mradi kwa muda fulani anapaswa kujiridhisha kuwa barabara anayopitisha vifaa anaitengeneza lakini hili limeshindwa kufanyika.”

Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema mpaka sasa mradi haujaonyesha dalili ya kuchelewa na kama itakuwapo watajitahidi kushughulikia.

“Suala la uharibifu wa miundombinu si Rufiji pekee, bali ni nchi nzima kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Mvua zikikatika wakandarasi wamejipanga kuanza ukarabati,” alisema Dk Kalemani.

Mikakati ya mkoa

Kuhusu athari za mvua hizo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo pia alisema Rufiji imeathirika zaidi kwa kuwa inapokea maji kutoka mito ya Kilombelo, Ruaha Mkuu na Ruengu inayokutania Bwawa la Nyerere na kwamba mabwawa ya Mtera na Kidatu yamejaa.

Alisema katika ziara yake wilayani Rufiji wananchi walimueleza kuwa eneo hilo liko chini na miaka ya nyuma walitakiwa wahame, jambo ambalo mkuu huyo wa mkoa alikubaliana nalo.

Alisema kuna eneo la ekari 150 za Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ambalo wanatakiwa walichukue ili litumiwe na wananchi.

Alisema amemuagiza mkuu wa wilaya na mkurugenzi wake wapime eneo la ekari 100 na kugawanya kwa wananchi na ekari 30 zitengwe kwa ajili ya kujenga kituo cha afya na nyingine 20 kwa ajili ya shule mbili.

Alisema jitihada zinafanyika kama kuzungumza na wadau mbalimbali ili watoe misaada ya kibinadamu kwa walioathirika.

Advertisement