Magufuli aahidi kuwaamsha watendaji wake wafikiri tofauti

Magufuli aahidi kuwaamsha watendaji wake wafikiri tofauti

Muktasari:

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi kupitia CCM, John Magufuli amesema atakapochaguliwa tena, atakwenda kuwaamsha wataalamu walio chini yake ili waanze kufikiria nje ya boksi katika utendaji wao

Dar es Salaam.  Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amesema atakapochaguliwa tena atakwenda kuwaamsha wataalamu walio chini yake ili waanze kufikiria nje ya boksi katika utendaji wao.

Ameyasema hayo leo jumatatu Oktoba 26 katika mkutano aliofanya katika jimbo la Kondoa wakati akimnadi mgombea ubunge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji akiwa njiani kuelekea Dodoma.

Magufuli amesema changamoto nyingine ikiwemo ya maji inaweza kutatuliwa kwa watendaji kujiongeza na kutumia vitu vilivyopo.

“Wakati mwingine wataalamu wangu wanakosa busara za kupanga na kufikiria, barabara hii yote ina madaraja yanapitisha maji, ukichukua madaraja yote haya ukayaelekeza sehemu fulani na kuchimba bwawa, likawa na maji mengi, ukaleta umeme ukafunga mtambo wa kupeleka maji juu katika tanki na kuyasambaza hatutakuwa na shida ya maji,”

“Lakini pia wataalamu wangu wakati mwingine wanashindwa kufikria nje ya boksi, kwa sababu ukileta vifaa vya kutengeneza barabara na kwenda katika bonde linaloleta maji mengi ukaziba tuta maji yanapokuwa yanakuja hayatapitiliza,”amesema.

“Yatajitenga na kuwa mengi, mifugo yetu itapata maji,  atayetaka kuogelea ataogelea, atakayetaka kufuga samaki atafuga mle na ndiyo maana nimejipanga katika safari nyingine mkinichagua niende nikawaamshe wataalamu wangu waanze kufikiria nje ya boksi,”

Alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi hao kuwachagua watu wa CCM ili atakapokuwa anapeleka mapendekezo wasiyapinge.

“Kwa sababu mkiletea wale wanaopinga hata ukimwambia huyu mwanamke mzuri oa atapinga, ukisema ulete vituo vya afya watu wanapata shida watapinga, tunataka tuongeze vifaa kwenye vituo vyetu, tunataka katika miaka mitano ijayo tulete madaktari na manesi ikiwezekana hata X ray mashine mfanye upasuaji hapa,” amesema

.