Magufuli aitaka sekretarieti Sadc kujitathmini

Rais John Magufuli akizungumza kwa ajili ya kuwakaribisha kwenye Mkutano wa 39 wa SADC unaoendelea jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi Agosti 17, 2019 amekabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na kuitaka sekretarieti ya jumuiya hiyo kujitathmini kuhusu ukuaji duni wa uchumi kwa nchi wanachama

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi Agosti 17, 2019 amekabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na kuitaka sekretarieti ya jumuiya hiyo kujitathmini kuhusu ukuaji duni wa uchumi kwa nchi wanachama.

Akizungumza katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo,  Magufuli amesema kama hakuna jitihada kubwa zitakazofanywa na sekretarieti itakuwa vigumu kufikia lengo husika.

Katika mkutano huo uliofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Magufuli amesema changamoto kubwa ni uchumi, kwamba nchi wanachama zinapaswa kutumia mafanikio ya kisiasa kufikia mafanikio ya kiuchumi.

“Malengo ilikuwa kufikia asilimia saba ya ukuaji uchumi kwa nchi husika lakini tupo mbali na malengo yetu kiuchumi. Kuna sababu nyingi uchumi wetu kudorora. Mei mwaka hii nilitembelea nchi tano za Sadc kwa bahati mbaya tatu kati yake zilikuwa zimekumbwa na njaa na zilikuwa kwenye mchakato wa kuagiza chakula kutoka nje.”

“Wakati huo Tanzania ilikuwa na tani milioni 3.5 za chakula cha ziada. Matatizo mengi kama haya sekretarieti inafaa kuyaangalia na itusaidie, naamini tungepata majibu kutoka kwao kwa nini miaka 10 uchumi wa pato la ndani unashuka,” amesema Magufuli.