Magufuli akataa ombi la wananchi pori la akiba kugeuzwa shamba

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amekataa ombi la wananchi wa kijiji cha Kanazi Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa la kutaka wapewe pori la akiba lililopo katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amekataa ombi la wananchi wa kijiji cha Kanazi Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa la kutaka wapewe pori la akiba lililopo katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo.

Rais Magufuli ametoa uamuzi huo leo Jumanne  Oktoba 8, 2019  wakati akizindua barabara ya Sumbawanga – Kanazi yenye urefu wa kilomita 75 kwa gharama ya Sh91.5 bilioni.

 Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya kilomita 245 kutoka Sumbawanga – Mpanda.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo aliinua bango lililoandikwa “Ombi la eneo la kulima Pori la Akiba Lwafi Kakoma.”

Rais Magufuli akaliona bango hilo na kusema hawezi kuruhusu wakalima kwenye pori la akiba kwa sababu mapori hayo ndiyo yanayoleta watalii nchini

“Anasema kero ya ardhi pori la akiba, yeye anataka mapori yote tuyamalize tukose watalii. Tumesema tunataka kuinua utalii wa kusini sasa tukimaliza mapori yote watalii hawatakuja huku tutakosa fedha za kujenga barabara,” amesema Rais Magufuli.

Amesema hawezi kugeuza mapori yote kuwa mashamba ya kilimo kwa sababu serikali inaingiza mapato yake kutokana na utalii. Amewataka wananchi hao kutafuta mashamba sehemu nyingine lakini siyo kulima kwenye pori hilo la akiba.

Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Kanazi yenye urefu wa kilomita 75 ulikamilika mwaka 2017 na kukabidhiwa Oktoba 2018.

Mfugale amesema fedha zote za ujenzi wa barabara hiyo zimetolewa na Serikali na mpaka sasa mkandarasi amelipwa Sh72.5 bilioni kati ya Sh91.5 bilioni anazotakiwa kulipwa kwa ujenzi wa barabara hiyo.

“Nikukumbushe tu kwamba mwaka 2015 ulifika katika barabara hii ukiwa waziri, ukakuta mradi unasuasua. Ukamwagiza mkandarasi akamilishe ujenzi huo ndani ya miaka miwili na kweli imekamilika ndani ya miaka miwili,” amesema Mfugale.