VIDEO: Magufuli alipolihutubia Bunge kwa takwimu

Magufuli alipolihutubia Bunge kwa takwimu

Muktasari:

Hili ni miongoni mwa matukio makubwa ambayo yalitokea kipindi tovuti ya Mwananchi pamoja na mitandao ya kijamii ilipofungiwa kwa miezi sita.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli Juni 16, 2020 alilihutubia Bunge ambapo hotuba yake ilitumia takribani saa 2: 30 kuelezea namna alivyotekeleza ahadi zake kwa watanzania kupitia ilani ya CCM 2015/2020 katika ngwe yake ya kwanza.

Kiongozi huyo aliingia madarakani Novemba 5, 2015 alitumia ushahidi wa takwimu zaidi kila alipokuwa akieleza mafanikio ya kila sekta.

Hili ni miongoni mwa matukio makubwa ambayo yalitokea kipindi tovuti ya Mwananchi pamoja na mitandao ya kijamii ilipofungiwa kwa miezi sita.

Hili ni moja la tukio lililotokea kipindi tovuti hiyo ilipofungiwa, ni Rais kulivunja bunge, ikiambatana na hotuba yake iliyojikita kueleza mafanikio ya miaka mitano ya uongozi wake, kwa kutumia takwimu.

Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake, sehemu kubwa ilikuwa ni takwimu, akilinganisha hali aliyoikuta mwaka 2015 katika sekta mbalimbali na ilivyo sasa.

Alisema hayo bungeni jiini Dodoma katika hotuba yake ya takribani saa 2:30 ya kulivunja Bunge la 11 iliyohudhuriwa na marais watatu waliomtangulia Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete viongozi wakuu wengine wa zamaani na sasa pamoja na wake zao.

Makofi, vigelele na hata vibwagizo vya nyimbo vilitawala wakati akitaja takwimu hizo.

“Kwa sababu ya ufinyu wa muda sitaweza kueleza sekta zote. Serikali imejitahidi kuimarisha sekta zote ili kukuza uchumi wa Tanzania,” katikati ya hotuba yake wakati akiendelea kutaja takwimu kuthibitisha mafanikio ya Serikali yake.

Alifikia hadi kutaja kuongezeka kwa urefu wa samaki wakati akieleza jitihada zilizofanyika katika sekta ya uvuvi.

“Katika uvuvi Ziwa Victoria, sangara wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020,” alisema na kupigiwa makofi.

“Na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimita 16 hadi urefu wa sentimita 25.2.

“Na hivyo samaki wetu kuanza kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la Ulaya. Na nyinyi ni mashahidi waheshimiwa wabunge ndege zimeanza kuja kuchukua samaki wetu kwa ajili ya kupeleka nje.

“Haya si mambo madogo Mheshimiwa Spika.”

Kuhusu sekta ya elimu, Rais alisema Serikali ilianza kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na hadi Februari mwaka huu ilikuwa imetumia Sh1.01 trilioni kwa ajili ya kugharamia elimu.

Katika kipindi hicho, alisema, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka huu; na za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi 5,330 mwaka huu.

Alisema Serikali imekarabati shule kongwe za sekondari 73 kati ya 89 zilizopo. Vilevile, imejenga mabweni 253, maabara 227 na kuongeza vifaa vya maabara 2,956.

Kadhalika,  alisema Serikali imeongeza vyuo vya ufundi kutoka 672 mwaka 2015 hadi 712 mwaka huu. 

Kuhusu elimu ya juu, alisema bajeti ya mikopo kwa wanafunzi imeongezeka kutoka Sh348.7 bilioni mwaka 2014/15 hadi Sh450 bilioni mwaka 2019/20.

“Waheshimiwa wabunge, naamini nitakuwa sijakosea nikisema kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya elimu,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wabunge kwa kugonga meza.

Katika sekta ya afya, Rais Magufuli alisema Serikali imeongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,769 zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda 3.

Kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, Rais alilipongeza Bunge kwa kuendelea na vikao wakati wa janga hilo, huku akimshukuru Mungu kwa kuliepusha Taifa na athari zake.

“Tumeweza mpaka sasa hivi kutatua kwa kiasi kikubwa, si tu kufanikiwa kuushinda ugonjwa huo bali pia kupunguza athari zake zikiwemo za kiuchumi,” alisema.

Alisema pamoja na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kubashiri kuwa asilimia 60 ya nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, uchumi wake utakuwa kwa asilimia hasi, lakini sisi hautakua kwa negative. Utakua kwa asilimia 5.5 na kuendelea.

Pia alizungumzia mafanikio katika ukusanyaji mapato, uboreshaji wa mazingira ya kibiashara, uboreshaji wa mahakama, uondoaji wa kero kwa wakulima, wafanyakazi, wavuvi wafugaji na wafanyabiashara pamoja na jitihada za kuondoa migogoro ya ardhi.

Pia alizungumzia mafanikio katika ongezeko la Pato la Taifa, kupunguza kwa kiwango cha umaskini, kuongezeka kwa ajira, ongezeko la mapato yatokanayo na madini na pia kukua kwa sekta ya sanaa, burudani na michezo.

Na sehemu zote alitumia takwimu kufananisha mafanikio ya mwaka 2015 wakati akiingia Ikulu na sasa.

“Kwa bahati nzuri, Watanzania wengi wameona na wanayajua. Hivyo nina imani kubwa kwamba Watanzania wataendelea kutuamini na kutupa dhamana ya kuendelea kuongoza nchi yetu katika vipindi vingine vijavyo,” alisema.

“Na Binafsi naamini kutokana na misingi imara tuliyoiweka ya ukuaji uchumi, uzoefu mkubwa tuliopata, endapo wananchi wataendelea kutumaini na kutuchagua kuongoza kwa miaka mitano ijayo, tutafanya mambo makubwa zaidi.”

Baada ya hotuba hiyo, Rais alitangaza kulivunja Bunge hilo hadi litakapoanza jingine kwa mujibu wa Katiba.

 Lakini hotuba hiyo haikukosa ukosoaji

 Mgombea ubunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema hotuba hiyo imepwaya kwa sababu imetazama nini ambacho wamefanikiwa kufanya na haikujali changamoto za kwenda mbele zinatatuliwa namna gani.

Alisema kwa maoni yake ilikuwa ni hotuba ya uchaguzi zaidi kuliko hotuba ya kulitazama taifa kwa ujumla wake. “Ukitazama hotuba nyingine zilizopita unaoiona hiyo tofauti,” alisema.

Mwingine aliyezungumzia hotuba hiyo ni Zuhura Muro, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Lindam Group Limited, ambaye alisema kuondolewa kwa tozo 60 katika mwaka ujao wa fedha kunaonyesha jinsi Serikali ya Magufuli ilivyopania kuboresha mazingira ya biashara.

Alimsifu Magufuli kwa kuongeza nidhamu katika kuendesha Serikali na jinsi sekta binafsi inavyofanya kazi.

“Kwa jinsi ilivyo, hali hii imeongeza kufuata sheria katika malipo yaa kodi,” alisema mwenyekiti huyo wa zamani wa bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

“Pale unaposimamia kodi kwa usahihi, unaondoa kero za kodi, kukubali kulipa kodi kunakuwa hakuepukiki na matokeo yake Serikali inapata fedha zaidi kwa ajili ya huduma za jamii na miradi ya maendeleo.”

Alisema uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati kutapunguza gharama katika biashara.

“Kwa hiyo nilichotaka kusema kutoka katika hotuba ya Rais ni kwamba naona mambo yanakwenda katika mwelekeo sahihi,” alisema Muro

Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Saleh alisema ilikuwa hotuba ambayo imepitia maeneo mengi, lakini ilikuwa ni hotuba ya kampeni.

Alisema Rais amejitahidi kuelezea mafanikio yote ambayo amefanikiwa na kwa kweli yako mambo mtu hawezi kukataa kwa sababu yanaoneka wazi.

Saleh alitoa mfano wa ujenzi wa reli ya kisasa akisema kwa upande wake anaona reli hiyo ingekuwa na manufaa zaidi kama ingekuwa na lengo la kubeba mizigo zaidi kwa kuwa faida ya usafiri wa reli ni mizigo.

Alisema hata kwenye usafiri wa anga ndege za kubeba mizigo ndio zingekuwa na faida zaidi kuliko kununua ndege zote za abiria na hasa katika kipindi hiki cha corona.

Saleh alisema miradi mingi inaokana kama ni mafanikio, lakini ingeweza kufanikiwa zaidi kama fedha za maendeleo zingepelekwa kwa ukamilifu wake.

Alisema maeneo mengi fedha za maendeleo zimeenda chini ya asilimia 40, isipokuwa baadhi ya miradi.

Kuhusu kudhibiti rushwa na matumizi mabaya ya fedha alisema hiyo si sawa kwa sababu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imekuja na taarifa mbaya kuhusu maeneo hayo.

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema hotuba ya Rais ya kufunga Bunge imeeleza utekelezaji wa shughuli ambazo amezifanya kwa muda wake wa miaka mitano.