Magufuli ampa mkandarasi mwaka mmoja

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amemtaka mkandarasi anayejenga Barabara ya Mbinga –Nyasa yenye umbali wa kilomita 67 kukamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja

Mbinga. Mkandarasi anayejenga Barabara ya Mbinga –Nyasa yenye umbali wa kilomita 67 kwa kiwango cha lami itakayogharimu Sh134.712 bilioni, ameagizwa kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi huo mwakani badala ya waka 2021.
Agizo hilo limetolewa jana na Rais John Magufuli kwa mkandarasi huo kampuni ya Chicco ya nchini China, akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara hiyo.

Rais Magufuli amesema anataka wananchi wapate huduma ya barabara mapema kabla hajamaliza awamu yake ya kwanza ya uongozi kwani anataka aifungue mwenyewe akiwa madarakani, huku akiwahakikishia kuwa fedha ya kuwalipa ipo.

"Njoo uahidi lini utakamilisha ujenzi wa barabara hii kwani nataka ujifunge mwenyewe sisi pesa tunazo na tunahitaji hii barabara ijengwe kisasa, ndio maana kilomita ni chache na pesa ni nyingi kutokana na hali halisi ya barabara kuwa na kona, tutapasua milima na kuipanua tunataka ijengwe kisasa zaidi ili wananchi wafanya biashara zao na kukuza uchumi," amesema Rais Mgufuli.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa mikoa ya Ruvuma na Mtwara na taifa kwa ujumla kwani utarahisisha shuguli za uchumi. Pia, utafungua fursa za biashara kwa wananchi na wajasiriamali wadogo hivyo amewataka kuitumia ili kuongeza kipato chao.

Pia, ameishukuru Benki ya Afrika (AfDB) kwa kufadhili mradi huo na amewaahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao na kulipa mkopo bila usumbufu huku ikidhibiti rushwa.

Naye kaimu mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), Crispinus Ako amesema ujenzi huo ulianza Aprili 3, 2018 na unatakiwa kukamilika Januari 21, 2021 na kwamba, tayari Sh21.299 bilioni zimeshalipwa.

Awali Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Isack Kamwele amsema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu ambayo itaziunganisha Mbinga, Mbambabay- Mtwara hivyo kukamilisha mtandao wa barabara yenye umbali wa kilomita 1,024.

Amesema mikoa yote ya kusini itakuwa imeunganishwa kwa barabara za lami hivyo kufungua fursa za kiuchumi kwa jamii na utalii nchini.

Naye mwakilishi wa AfDB, Dk Alex Mibiru amesema amefarijika kuhudhuria uwekaji wa jiwe la msingi kwenye barabara hiyo kwani mradi huo ni wa kihistoria na ameahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali na kuwasaidia Watanzania.