Magufuli asema alitamani kufukuza viongozi wote wa Morogoro

Muktasari:

Rais Magufuli asema mkoa wa Morogoro umekuwa na changamoto mbalimbali za kiuongozi na alitamani kuwafukuza kuanzia mkuu wa mkoa hadi mtendaji kata na kuwapeleka viongozi wengine.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema mkoa wa Morogoro ni kati ya mikoa iliyowasumbua kuiongoza na alitamani uwe mkoa wa mfano kwa kuwafukuza watendaji kuanzia mkuu wa mkoa hadi mtendaji kata.

Ameeleza hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 Ikulu Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua Septemba 20,2019 akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare aliyechukua nafasi ya Dk Stephen Kebwe.

“Namshukuru Dk (Stephene) Kebwe yupo hapa, lakini ukweli bila unafiki kama kuna mkoa uliotusumbua katika kuongoza ni Morogoro. Mambo mengi katika mkoa huo, hayakwenda, nisiposema nitaonekana ni mnafiki na sipendi hivyo,” amesema  Rais Magufuli.

Amesema mkoa huo ungekuwa demo kwa kuwatimua watendaji wote kisha kuteua wengine.

Magufuli ametolea  mfano katika halmashauri za mkoa huo kuwa  matumizi ya fedha ni ovyo na alishatuma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kufuatilia akabaini changamoto hizo huku ujenzi wa vituo vya afya havikamiliki wakati fedha zipo.

“Migororo ya ardhi haishi, kuna wawekezaji wa kiwanda cha Tumbuka wanataka kuondoka. Tulianza kuondoa wakurugenzi tulianza na wa Malinyi, tukadhani tumetibu kumbe hakuna, tukamtoa hadi wa halmashauri wa Morogoro Vijijini,” amesema

“Ukishaona mkuu wa wilaya na mkurugenzi wanagombana kisa maslahi, mkuu wa mkoa hujawahi kukemea wala kuchukua hatua maana yake hautoshi. Dk Kebwe nampenda sana by profession (taaluma) ni dokta, lakini katika uongozi wa mkoa ulimshinda,” amesema

Amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikwenda Morogoro na kumweleza kuwa kuna shida katika mkoa huo.

Magufiuli amesema haiwezekani watendaji wa chini wa mkoa wanafanya kazi vibaya halafu mkoa wa mkoa ukajisifu.

 “Haiwezekani ukawa waziri lakini watendaji wako wa chini hawafanyi kazi vizuri haiwezekani. Ndio maana tulibadilisha kwa kumteua mwenyekiti wa CCM Arusha (Sanare) najua nampeleka sehemu yenye changamoto na huu ni mtego,” amesema

Amesema Sanare anawajua wafugaji ni watu gani, inawekana na yeye akawa mfugaji ndiyo maana amepelekwa huko akatatue matatizo ya wafugaji kulisha mifugo kwenye mashamba na wakulima kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya wafugaji.

“Nataka ukatatue pia migogoro ya halmashauri, baadhi ya wakurugenzi wanachangisha fedha kwa ajili ya kupeleka makao makuu, ndiyo maana baadhi ya miradi haiendi.”

“Unapeleka Sh1.3 bilioni za kujenga hospitali ya wilaya inakaa miezi hata jengo halijajengwa, tunawanyima haki wananchi,” amesema.