Magufuli asema ruksa wakulima kupandisha bei ya mahindi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Serikali haiwezi kupanga bei elekezi ya mazao na kuwataka wakulima kupandisha bei ya mahindi kulingana na mahitaji ya soko.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Serikali haiwezi kupanga bei elekezi ya mazao na kuwataka wakulima kupandisha bei ya mahindi kulingana na mahitaji ya soko.

Ameeleza hayo leo Jumatano Novemba 20, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa  Gairo mkoani Morogoro akiwa njiani kwenda jijini Dodoma.

“Tuendelee kuchapa kazi mvua zimeanza kunyesha na Gairo kuna wakulima wazuri  chapeni kazi. Asiyefanya kazi na asile, narudia Serikali haitaingilia bei ya mazao ya wakulima,” amesema.

Amesema wakati bei ya mahindi ikishuka Serikali haiwezi kuingilia kupanga na kupandisha bei hiyo ikiwemo ya mahindi.

“Haiwezekani Serikali kupanga bei ya mahindi itakuwa imefilisika kutawala. Hii ni kwa sababu bei ya mahindi inapoteremka Serikali haiingilii kupanga ili ipande kwa hiyo yakipanda bei haiwezi kuingilia ili ishuke.”

“Serikali ninayoiongoza haitapanga bei ya mahindi, yatajiendesha kwa soko na huu ni wakati wa wakulima, pandisheni tu, anayeona mahindi yamekuwa ya bei ya juu aende akalime ya bei ya chini,” amesema.

Amebainisha kuwa kuna soko kubwa la mahindi katika nchi za jirani na kuwataka wakulima kutumia fursa hiyo.

“Tanzania tuna soko kubwa la watu 450 milioni ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), wakulima ndugu zangu tumieni nafasi hiyo,” amesema Magufuli.