Magufuli azindua barabara Katavi

Muktasari:

Rais  wa Tanzania, John Magufuli Alhamisi Oktoba 10, 2019 amezindua ujenzi wa barabara ya Stalike – Mpanda yenye urefu wa kilomita 39 na barabara ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilomita 359 itakayounganisha Mikoa ya Katavi na Tabora.

 

Dar es Salaam. Rais  wa Tanzania, John Magufuli jana Alhamisi Oktoba 10, 2019 amezindua ujenzi wa barabara ya Stalike – Mpanda yenye urefu wa kilomita 39 na barabara ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilomita 359 itakayounganisha Mikoa ya Katavi na Tabora.

Pia, Rais Magufuli amezindua kituo cha mabasi cha Mizengo Pinda kilichopo katika mji wa Mpanda.

Kituo hicho kimepewa jina la Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambaye ni mzaliwa wa Katavi na alikuwa mbunge wa Mpanda Vijijini.

Akiwa kwenye uzinduzi huo kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli amezungumza na wananchi na kuwashukuru kwa kumpigia kura yeye pamoja na wabunge na madiwani ili wafanye kazi ya kuwaletea maendeleo.

“Haya ndiyo matokeo ya kura zenu mlizopiga. Ninachotaka muendelee kufanya kazi, mengine mtuachie Serikali,” amesema Rais Magufuli.

Mkuu huyo wa nchi amewataka wananchi mkoani humo kujitokeza kujiandaa kuchagua viongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Amewapongeza wananchi wa Mpanda kwa maendeleo makubwa wanayoyafanya na kuwataka waitunze stendi ya mabasi na waitumie vizuri kujiletea maendeleo yao.