Magufuli kufungua mkutano wa Ma IGP kutoka nchi 14 Arusha

Friday September 13 2019Rais wa Tanzania, John Magufuli

Rais wa Tanzania, John Magufuli 

By Bertha Ismail, Mwananchi

Arusha. Rais wa Tanzania, John Magufuli anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa 21 wa shirikisho la wakuu wa polisi wa nchi za  Afrika Mashariki Septemba 19, 2019 jijini Arusha.

Mkutano huo utashirikisha wajumbe ambao ni ma Inspekta Jenerali wa Polisi kutoka nchi 14 za  Burundi, Comorro, Djibouti, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na mwenyeji Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha nchini Tanzania leo Ijumaa, Septemba 13,2019, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Tanzania, David Misime amesema maandalizi yote ya mkutano yamekamilika na wanaanza kupokea wageni  kuanzia leo.

Misime amesema kabla ya ufunguzi wa mkutano huo kutakuwa na vikao vya wakuu wa vitengo vya Interpol utakaofanyika kati ya Septemba 15 hadi  17,2019 kisha kufuatiwa na mkutano wa wakurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) na kikao cha wajumbe wa kamati ndogo ya mafunzo.

 Amesema kutakuwa na kikao cha kamati ndogo ya wataalamu wa sheria, vikao vya wajumbe wa kamati ya dawati la maswala ya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kikao cha  wajumbe wa masuala ya kukabiliana na ugaidi nchini.

Misime amesema mkutano huo utakaokuwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka"  ukiwa na  lengo la kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na makosa yanayovuka mipaka na kuweka mikakati ya pamoja katika maazimio ya kukabiliana na uhalifu wa kuvuka mipaka.

Advertisement

“Katika mkutano huu, Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania  Simon Sirro atakabidhiwa uenyekiti wa shirikisho la wakuu wa polisi wa nchi za Afrika Mashariki,” amesema Misime.

Amesema katika mkutano huo, watatenga siku moja ya kuwapeleka wageni hao katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi Moshi (CCP) mkoani Kilimanjaro kuangalia madarasa na mabweni mapya yaliyojengwa na Serikali na wadau ili kuleta wanafunzi wao wa polisi kujifunza.

 

 

Advertisement