Video yaonyeshwa kesi ya kina Mbowe

Monday August 19 2019

Katibu Mkuu , Chadema, Dk Vicent Mashinji,Koplo Charles,mwenyekiti,Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ,Freeman Mbowe,

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe  

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu imeonyeshwa ushahidi wa video uliowasilishwa na shahidi wa sita, katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Video hiyo ilitolewa leo Jumatatu Agosti 19, 2019 mahakamani hapo na shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, ambaye ni askari polisi mwenye namba F 5392 Koplo Charles, wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao

Ushahidi huo wa video umeonyeshwa  mahakamani hapo kwa kutumia ‘Projector’ katika chumba cha mikutano na mafunzo cha Tehama kilichopo Kisutu, baada ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, kuamuru video hiyo ionyeshwe.

Kabla ya kuonyesha kwa video hiyo, Hakimu Simba alitoa uamuzi wa kuiruhusu video hiyo ionyeshwe na kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi wakipinga kuonyeshwa kwa  video hiyo.

Hata hivyo, wakati video hiyo ikionyeshwa katika ukumbi huyo, washtakiwa na watu wengine walikuwa kimya wakisikiza ile kilichokuwa kinaonyeshwa

Katika video hiyo, iliyochukua saa  moja na dakika 21, ilionyesha viongozi hao wakihutubia wananchi wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni uliofanyika Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui vilivyopo Mwananyamala.

Advertisement

Koplo Charles alionesha video ya kwanza aliyoipa jina la Mkutano wa Chadema wa mwaka 2018 ambayo ilionesha baadhi ya  viongozi na wabunge wa Chadema wakiongozwa na  Freeman Mbowe na  Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji wakimnadi Salum Mwalimu aliyekuwa mgombea ubunge katika uchaguzi huo.

Video hiyo yenye mikanda miwili, ulianza kuwekwa mkanda wa kwanza uliochukua  dakika 56: 37, ambao katika mkanda huo, ulionyesha  wabunge kadhaa wa Chadema akiwemo, John Heche (Tarime Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Halima Mdee (Kawe) Ester Bulaya (Bunda Mjini) Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) wakitoa hotuba zao za kumnadi Salum Mwalimu.

Video hiyo pia, ilimuonesha Mbowe akihutubia wananchi waliohudhuria katika mkutano huo na kisha kumkaribisha Mwalimu kwa ajili ya kunadi sera zake.

Baada ya kuisha mkanda wa kwanza, Koplo Charles aliweka mkanda wa pili uliochukua dakika 25:55, ambao ulionyesha  Mbowe akihutubia kisha kuhamasisha wananchi kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Kinondoni.

Katika video hiyo, Mbowe alisikika akisema  kuwa Raisi (John) Magufuli ni mwepesi kama karatasi, hiyo Mbowe ataongoza mapambano katika kudai Haki.

Mahakama baada ya kumaliza kuangalia video hiyo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo kwa  muda wa dakika 30 na baada ya hapo  kesi hiyo  itaendelea na ushahidi ambapo Koplo Charles ataendelea kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

 


Advertisement