Majaliwa alivyozungumzia gharama za utalii Tanzania

Saturday January 18 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Zanzibar. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza wadau wa masuala ya utalii nchini wafanye mapitio ya gharama za huduma wanazowatoza watalii na amesisitiza si sahihi kuwatoza wazawa kwa kutumia fedha za kigeni au gharama sawa na wageni. 

Aliyasema hayo jana Ijumaa, Januari 17, 2020 wakati akizungumza na wanachama wa Umoja wa Wenye Mashamba Jozani (Uwemajo) mara baada ya kukagua miradi ya umoja huo. 

Waziri Mkuu alisema kuna baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za kitalii wazawa wanatozwa gharama sawa na wageni. Hivyo, aliwasisitiza waandae viwango maalumu kwa ajili ya wazawa ili kuhamasisha utalii wa ndani. 

Alisema ni lazima wadau hao wakatengeneza mazingira mazuri yatakayowavutia wazawa kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii nchini. “kitendo cha kuwatoza wazawa gharama sawa na wageni kitasababisha baadhi kushindwa kutembelea maeneo hayo.” 

Akiwa katika eneo hilo, Majaliwa alisema amefurahishwa na namna ambavyo umoja huo unavyotunza mazingira pamoja na viumbe maliasili nyingine kama kobe, kasa, samaki na hivyo kulifanya eneo hilo kuwa kivutio cha utalii. 

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi hao kuendeleza ushirika wao huo kwa sababu utawawezesha kupata mikopo pamoja na misaada mingine kama elimu kuhusu kilimo bora. 

Advertisement

Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha wakulima wananufaika kutokana na kilimo chao. Aliongeza kuwa ushirika unapaswa kuwa chachu ya mafanikio, hivyo, amewapongeza wananchi hao kwa kuwa na ushirika imara. 

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwasisitiza wananchi watumie ipasavyo vyandarua vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa malaria. Aliyasema hayo wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Kizimkazi Dimbani, Wilaya ya Kusini.  

Waziri Mkuu akiwa wilayani humo alishiriki maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kijiji kwa kugawa vyandarua kwa wanawake wajawazito. Wakati akigawa vyandarua hivyo, alisisitiza umuhimu wa kutumia vyandarua kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuvitumia kama uzio katika bustani za mbogamboga.

Advertisement