Majaliwa ataka utashi wa kisiasa kupambana na uhalifu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza leo wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa SADC wa Sekta ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa jijini Dar es Salaam leo

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua mkutano wa 21 wa wakuu wa polisi, Mashariki mwa Afrika na kuwataka kukabiliana na uhalifu licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wanasiasa katika nchi za Mashariki mwa Afrika kuwa na utashi wa kisiasa katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka ili kuufanya ukanda huo uwe salama.

Akifungua mkutano wa 21 wa Shirikisho la wakuu wa majeshi ya polisi, katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika(EAPCCO) leo Alhamisi Septemba 20, 2019  Majaliwa amesema kama kukikosekana utashi wa kisiasa ni vigumu kukubaliana na uhalifu katika nchi wanachama.

Amesema wa utashi wa  kisiasa ni muhimu sana katika kupambana na uhalifu na akawataka wanasiasa wengine kutoa ushirikiano kwa vyombo hivi ili vitimize wajibu wake.

Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na uhalifu pia  pia kuna changamoto ya utofauti wa sheria ambao unaweza kutoa mwanya kwa wahalifu kukimbilia nchi moja hadi nyingine.

"Ili kudhibiti uhalifu ukiwepo wa biashara ya dawa za kulevya sote tunapaswa kuwa na sheria kali zinazofanana ili kuzuia mhalifu kutoka nchi moja na kukimbilia nyingine na akawa salama," amesema

Waziri Mkuu amempongeza mwenyekiti aliyemaliza muda wake kwa kufanya kazi nzuri katika kipindi chake licha ya kukabiliwa na majukumu mengi.

Akizungumzia kuteuliwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania (IGP) Simon Sirro kuongoza shirikisho hili alimtaka kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, Mkuu wa polisi wa Sudan, Luteni Generali Idil Mohamed  Bashir

Waziri Mkuu amemtaka IGP Sirro kuendelea kuimarisha ushirikiano na umoja wa EAPCCO  katika  kusimamia utekelezaji wa maazimio na malengo ili kuleta manufaa zaidi katika umoja huo.

Waziri wa Mambo wa Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na uamuzi wa mkutano huo ili kuhakikisha ukanda wa Mashariki mwa Afrika unaendelea kuwa salama.