Majaliwa atoa ombi kwa Japan kuzisaidia nchi za Afrika

Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Filippo Grandi kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania yakiendelea, Yokohama, Japan.

Muktasari:

Japan imeombwa kutafuta suluhu ya kudumu ili Afrika iweze kuondokana na changamoto ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabia nchi, ukame, njaa na magonjwa.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa rai kwa nchi ya Japan kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto ambazo bado zinazikumba nchi za Afrika ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabianchi, ukame, njaa na magonjwa.

Hiyo ni kutokana na Tanzania kuendelea kuwa kimbilio la watu wengi wanaopisha machafuko katika nchi zao ambapo hadi Agosti 1, 2019 kulikuwa na wakimbizi 305,983 nchini humo. 

Taarifa kwa umma  iliyotolea na ofisi yake leo Ijumaa Agosti 30,2019 imesema Majaliwa ameyasema hayo kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu kuimarisha amani na usalama barani Afrika uliofanyika nchini Japan wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7).

Mbali na kuzisaidia nchi za Afrika pia ameitaka nchi hiyo kujitolea kuchangia na kuwekeza kwenye miradi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira yaliyoharibiwa kutokana na uwepo wa kambi za wakimbizi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na kubadilishana teknolojia hususan maeneo ya mipakani na mifumo ya kutoa taarifa mapema kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza itasaidia kuboresha mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na wakimbizi na watu wanaotafuta makazi.

“Uwepo wa wakimbizi na watu wanaotafuta makazi kwa namna moja au nyingine huathiri mazingira, jamii usalama na uchumi wa nchi inayowapokea. Hivyo ni ombi letu kwenu kushirikiana nasi kwenye miradi mbalimbali katika kuboresha mazingira” amesema Majaliwa

Amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kimbilio kwa wakimbizi kutoka nchi jirani wanaokimbia nchi zao kutokana na migogoro ya kisisasa, kikabila na kuibuka kwa vikundi vya uasi huku akibainisha kuwa  Agosti 1, 2019, Tanzania ilikuwa inahifadhi wakimbizi.

Katika mkutano huo Majaliwa alifanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Fillipo Grandi ambapo walikubaliana usalama kwenye makambi ya wakimbizi, mipaka pamoja na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na Wakimbizi.