Majaliwa awasimamisha watumishi nane Morogoro, aagiza wafikishwe kortini

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameendelea na ziara mkoani Morogoro ambapo akiwa Ulanga amewasimamisha watumishi nane kwa ubadhirifu wa Sh3 bilioni na kuagiza wafikishwe mahakamani.
  •  Jana Jumapili, Majaliwa alitangaza kuwasimamisha watumishi saba wa Halmashauri ya Kilombero na Mji Ifakara mkoani humo kwa ubadhirifu wa Sh1.3 bilioni huku akiagiza fedha hizo kurejeshwa ndani ya siku tatu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi wanane  wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya Sh3 bilioni za mapato ya ndani.

Amesema watumishi wa umma wanawajibu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu. “Nawasihi nyote muache kufanya kazi kwa mazoea, mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano na anayejiona hatoshi ajiondoe.”

Taarifa iliyotumwa na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi hao leo Jumatatu, Septemba 16, 2019 wakati akizungumza na watumishi na madiwani  wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo mjini Mahenge.

Watumishi hao kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Yusuph Semguruka ambaye kwa sasa amehamishiwa Tamisemi, Rajabu Siriwa (mwekahazina), Stanley Nyange, Jonson Mwenyembole, Isack Mwansokope, Said Majaliwa, Charles Steven na Hezron Lopa.

Pia, Waziri Mkuu ametumia kikao hicho kumrejesha kazini na kumpandisha kuwa mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Agustine Mwaria ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi na kuibua ubadhilifu huo. Baada ya kuibua ubadhilifu huyo mtumishi huyo alisimamishwa kazi.

Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi pamoja na kujiepusha na vitendo vya wizi kwa sababu wanaoathirika baada ya wao kuchukuliwa hatua za kisheria ni wenza wao na watoto.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya amesema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto wa ubadhilifu wa fedha za umma hali inayosababisha kuwepo kwa mpasuko kati ya watumishi na Baraza na Madiwani.

Amesema watumishi wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo wanaandamwa.

Majaliwa yuko mkoani Morogoro kwa ziara ya siku tano aliyoianza juzi Jumamosi Septemba 14, 2019 ambapo jana Jumapili aliwasimamisha watumishi saba wa Halmashauri Mji wa Ifakara na Kilombero kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh1.3 bilioni alizoagiza zirejeshwe ndani ya siku tatu.