VIDEO: Majeruhi watatu ajali ya Morogoro watoka wodini, ICU abaki mmoja

Thursday September 12 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Majeruhi watatu kati ya 11 wa ajali ya lori la mafuta ya  petroli lililoangika kisha kulipuka moto eneo la Msamvu mkoani Morogoro ambao walikuwa wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam wameruhusiwa kutoka hospitalini.

Ajali hiyo ilitokea asubuhi ya Jumamosi Agosti 10, 2019 ambapo hadi leo Alhamisi Septemba 12,2019 vifo vilivyotokana na mlipuko wa moto huo ni 104.

Majeruhi walioruhusiwa leo Alhamisi ni kati ya 47 waliofikishwa Muhimbili kwa matibabu lakini 36 walifariki kwa nyakati tofauti na kubaki 11 wakiendelea na matibabu.

Daktari bingwa wa upasuaji, Edwin Mrema amesema wanawaruhusu wagonjwa hao watatu baada ya kupata nafuu kubwa lakini wataendelea kuwaangalia kupitia kliniki.

Amesema kwa sasa wamebaki majeruhi nane na mmoja pekee ndiyo yupo kwenye chumba uangalizi maalum (ICU) na waliosalia wapo kwenye wodi ya kawaida.

Dk Mrema amesema majeruhi aliye ICU anaendelea kuwa kwenye uangalizi kutokana na athari alizozipata.

Advertisement

“Huyu aliungua sana kwenye miguu, tukaona kadiri siku zinavyozidi kwenda hali yake inakuwa mbaya, tukaamua kumfanyia upasuaji kumuondoa miguu yote miwili na anaendelea vizuri,” amesema

Mmoja wa majeruhi hao, Shaban Abdalla ameeleza jitihada kubwa zilifanywa na madaktari kuokoa maisha yao hivyo wana kila sababu ya kushukuru.

“Nashindwa hata cha kuzungumza, tulikuja tukiwa na hali mbaya sana, siamini leo tumepona na ninarudi nyumbani naishukuru Serikali, madaktari na wauguzi wa Muhimbili,” amesema

Advertisement